Xi ahimiza utatuzi wa amani wa suala la Korea Kaskazini
12 Aprili 2017
Vyombo vya habari vya taifa nchini China vimesema Jumatano kwamba viongozi hao wawili walizungumza kwa njia ya simu katika kile kinachoonekana dhahiri kuwa ni juhudi za kuepuka kuipalilia zaidi hali hiyo baada ya Trump kuweka katika eneo hilo manowari zinazongozwa na meli yenye kubeba ndege za kivita kuonyesha nguvu zake.
Manowari hizo zimeelekea katika kanda hiyo na onyo jipya kwamba serikali ya Marekani iko tayari kupambana na Korea Kaskazini peke yake iwapo serikali ya China itakataa kusaidia kudhibiti tamaa ya jirani yake huyo kumiliki silaha za nyuklia.
Hadi sasa serikali ya Korea ya Kaskazini imejibu kama kawaida yake kwa kiburi cha ukaidi ikisema kwamba iko tayari kupambana katika vita vya aina yoyote ile vitakavyochaguliwa na Marekani na hata kutishia kwamba itafanya shambulio la nyuklia dhidi ya maeneo ya Marekani.
Vitisho hivyo vya kijeshi vimeitia wasiwasi China ambapo imeweka wazi kuvunjika moyo kwake na ukaidi wa serikali ya Korea Kaskazini lakini kipaumbele chake kimeendelea kuwa kuzuwiya mripuko wowote ule wa kijeshi ambao utaleta machafuko na ukosefu wa utulivu katika eneo hilo.
Ufumbuzi wa amani
Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya China katika mazungumzo yake ya simu na Trump, Xi amesisitiza kwamba China inatetea kulitafutia ufumbuzi suala hilo kwa njia ya amani.
Msemaji wa wizara ya mambo y anje ya China Lu Lang amesema mazungumzo hayo ya simu kati ya Xi na Trump yamesisitiza umuhimu wa kutatuwa mvutano juu ya suala hilo kwa njia ya amani.
Lang amesema"Bila ya shaka pande zote mbili zimezungumzia wasi wasi wao wa pamoja katika masuala ya kimataifa na kanda likiwemo suala la nyuklia katika rasi ya Korea na suala la Syria .Katika suala la nyuklia katika rasi ya Korea Rais Xi amesisitiza msimamo wa China wa kuheshimu lengo la kuondowa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea na kuendelea kulitafutia ufumbuzi suala hilo kwa njia ya amani kupitia majadiliano na mazungumzo."
Hapo jana rais wa Marekani aliandika kwenye mtandao wa twitter kwamba Korea ya Kaskazini inajitafutia matatizo na ikiwa China itaamua kusaidia hilo litakuwa jambo jema lakini ikiwa haitofanya hivyo watalitatuwa tatizo hilo bila ya wao.
Hofu za Marekani
Mfululizo wa hivi karibuni wa majaribio ya makombora wa Korea Kaskazini umeongeza hofu za Marekani kwamba serikali ya nchi hiyo yumkini hivi karibuni ikawa imeunda makombora yatakayoweza kufika katika mabara mengine yaani ndani ya ardhi ya Marekani pindi yakifyatuliwa na yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia.
Kuna tetesi kwamba Korea Kaskazini inajiandaa kuzinduwa ufyetuaji wa kombora au hata jaribio jengine la silaha za nyuklia kuadhimisha miaka 105 ya kuzaliwa kwa muasisi wa taifa hilo Kim-Il Sung hapo Jumamosi.
Katika mahojinao na mtandao wa kibiashara wa Fox Trump ameonya wana kundi la manowari ambazo zina nguvu sana kwamba wana nyambizi ambazo zenye nguvu kubwa sana kuliko hata meli yenye kubeba ndege za kivita.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Korea Kaskazini amesema hatua zisizo za busara za Marekani kutaka kuivamia nchi hiyo zimefikia hatua ya hatari.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP
Mhariri :Josephat Charo