1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano makali bado yaripotiwa mjini Hassakeh

Mjahida 22 Agosti 2016

Wapiganaji wa Kikurdi kaskazini mwa Syria wametolea mwito wapiganaji watiifu kwa Rais Bashar al-Assad kuweka chini silaha zao na kujisalimisha kufuatia wapiganaji hao wa kikurdi kupiga hatua katika mji wa Hassakeh

https://p.dw.com/p/1Jn7z
Kämpfer von der Kurdenmiliz YPG
mmoja ya wapiganaji wa kitengo cha ulinzi wa raia Syria YPGPicha: Imago

"Kwa wanamgambo wote wa serikali waliyozingirwa, sasa mnalengwa na vikosi vyetu, walenga shabaha na silaha zetu,” kilisema kitengo cha ulinzo wa raia nchini Syria YPG. “Hatutarejea nyuma, vikosi vyetu vinaelekea mjini, tunawatolea mwito muweke silaha chini na kujisalimisha katika makao makuu ya usalama yaliyoko karibu nanyi,” kiliongeza kitengo hicho cha ulinzi wa raia.

Maeneo mengi ya mji wa Hassakeh yanakaliwa na vikosi vya YPG lakini vikosi vya rais Bashar al Assad na wanamgambo waliyotiifu kwa serikali wanaendelea kudhibiti baadhi ya maeneo ya mji huo. Idriss Nassan, afisa mkuu wa Wakurdi amesema kundi hilo limechukua udhibiti wa maeneo mengi mjini humo hasa katika eneo jirani Ghwarian na baadhi ya miji ya  mashariki ya Nashwa na al -Hassakeh. Hata hivyo, bado mapigano makali yameripotiwa kuendelea katika maeneo hayo.

Syrien Präsident Bashar Assad
Rais Bashar al Assad wa SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Wiki iliyopita ndege za kivita za serikali ya Syria zilivurumisha mabomu kwenye  ngome zinazoshikiliwa na wakurdi mjini al Hassakeh kwa mara ya kwanza katika historia ya vita  vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo vinavyoendelea kwa miaka mitano sasa. Mapigano yalipamba moto kati ya vikosi vilivyotiifu kwa serikali na wanajeshi wa Kikurdi, wanaoungwa mkono na Marekani katika vita vyao dhidi ya wanamgambo wanaojiita dola la kiislamu. Aidha Marekani imetoa onyo kwa serikali ya Syria kutowatisha washirika wake kwa ndege za kivita.

Wakurdi wanaochangia silimia 10 ya raia wa Syria milioni 22.4 kabla ya vita, wamekuwa wakilalamikia ubaguzi chini ya utawala wa chama cha rais Assad cha Baath, chama cha kizalendo chakiarabu kuanzia mwaka 2011 wameendeleza jitihada zao za kujitawala.

Kwa upande mwengine mwanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Uturuki, inayopambana kivyake na uasi kutoka kwa wapiganaji wa kikurdi, inawasiwasi juu ya uenezaji wa kikosi cha wakurdi katika moja ya mipaka yake. Kwa sasa Uturuki imeridhia kikundi cha  jeshi huru la Syria kujikusanya katika ardhi yake ili kushambulia kijiji kinachoshikiliwa na  wanamgabo wa dola la kiislamu kwa lengo la kuwanyima nafasi au udhibiti kundi la YPG.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef