1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yazindua mikakati ya kupambana na Saratani ya kizazi

17 Novemba 2020

Shirika la Afya Duniani WHO siku ya jumanne limezindua mkakati mpya wa kupambana na kuiangamiza Saratani ya kizazi, kwa matumizi mapana ya chanjo, vipimo vipya na matibabu ili kuokoa maisha ya watu kufikia mwaka 2050.

https://p.dw.com/p/3lOiD
Genf Tedros Adhanom Ghebreyesus, Generealdirektor WHO | Ebola-Ausbruch Kongo
Picha: Reuters/D. Balibouse

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, awali ilikuwa kama ndoto kupambana na kuondoa kabisa aina yoyote ya saratani lakini sasa shirika hilo limejihami na zana za gharama nafuu na za kutosha kukabiliana na Saratani. Saratani yaongezeka duniani 

Mkatati huo umetoa mwito kwa mataifa mbalimbali kutoa chanjo ya saratani ya kizazi angalau kwa asilimia 90 ya wasichana walio chini ya umri wa miaka 15 kufikia mwaka 2030. Aidha WHO katika mkakati wake mpya imetoa wito kwa angalau asilimia 70 ya wanawake kuhakikisha wanapimwa saratani ya kizazi wanapofikisha umri wa miaka 35 na kisha kupima tena wanapofikia umri wa miaka 45 na angalau asilimia 90 ya waliopatikana na ugonjwa huo wanapokea matibabu.

Erster Impfstoff gegen Krebs in Australien getestet
Chanjo ya kwanza ya saratani iliyojaribiwa Australia - Sophie Weisz (14) wakati akidungwa sindano ya chanjo ya saratani ya kizazi, huko Sydney.Picha: picture-alliance

Makubaliano ya kutumia chanjo

Zaidi ya wanawake nusu milioni duniani wanapimwa na kupatikana na saratani kila mwaka, huku mamia kati yao wakifariki kutokana na ugonjwa huo. Kwa mujibu wa WHO iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa idadi itaendelea kuongezeka.

Wiki iliyopita WHO katika mkutano wake wa kila mwaka unaowajumuisha wanachama wake kutoka mataifa 194 walikubaliana kubuni mbinu za kuangamiza saratani. Soma zaidi Saratani yawakumba wengi Kenya

Princess Nothemba Simelele Mkurugenzi msaidizi wa WHO amesema wamepiga hatua kubwa na kwa mara ya kwanza dunia imekubaliana kuitomeza kabisa saratani ambayo inaweza kuepukika kwa kutumia chanjo na pia inaweza kutibika iwapo itagunduliwa mapema.

Hata hivyo WHO imesema kuna mipango mizuri ya kurahisisha upimaji, kupunguza gharama na upatikanaji wa matibabu licha ya mkakati huu mpya kuzinduliwa wakati ulimwengu umejikita katika kupambana na janga la virusi vya Covid-19.

Simelele amesema janga la Corona limevuruga mpangilio wa chanjo, upimaji na matibabu ya saratani ya kizazi na kufungwa kwa mipaka katika mataifa mbalimbali kumepunguza upatikanaji wa dawa.

Aidha shirika la Afya Ulimwenguni linasema kutoa chanjo kwa wasichana 9 kati ya kumi walio chini ya umri wa miaka 15, kuboresha upimaji na matibabu kwa wanaogua kunaweza kupunguza athari ya saratani ya kizazi kwa asilimia 40 na kuzuia vifo vya takribani wanawake milioni 5 kufikia mwaka 2050.

 

AFP/Rtre