WHO yapindukia malengo ya chanjo ya polio Gaza
3 Septemba 2024Kwenye awamu hii ya kwanza ya siku 10 iliyoanza Jumapili (Septemba 3), WHO inasema imefanikiwa kugawa chanjo kwa zaidi ya watoto 161,000, kikiwa kiwango cha juu kabisa kwa siku mbili za mwanzo.
Mwakilishi wa shirika hilo kwenye mamlaka za Palestina, Rik Peeperkorn, aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, kwamba wanadhamiria kuwapatia chanjo asilimia 90 ya watoto wa Gaza ili kuepusha uwezekano wa kusambaa kwa maradhi hayo, ambayo yanaweza kusababisha ulemavu wa kudumu, kupooza na hata kifo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Soma zaidi: Netanyahu alemewa na shinikizo kufikia makubaliano
Peeperkorn alisema lengo lao ni kuwachanja watoto 640,000 kwenye ukanda huo ambao eneo lake kubwa limegeuzwa kuwa vifusi, na sehemu kubwa ya wakaazi wake milioni 2.4 wamelazimika kuyahama makaazi yao kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel na kukimbilia kwenye maeneo machafu, ambayo ugonjwa wa polio unahofiwa kuweza kusambaa kwa kasi.
Kampeni ya chanjo ilianza katikati mwa Gaza ambako kuna idadi kubwa zaidi ya wakaazi, ambako WHO awali ilikuwa imepanga kuwachanja watoto 156,600 walio chini ya miaka 10.
Siku ya Alkhamis, kampeni ya chanjo inatazamiwa kuhamia upande wa kusini ambako watoto 340,000 wanatarajiwa kuchanjwa na kisha upande wa kaskazini ambako watachanjwa watoto 150,000 kwenye awamu hii ya kwanza.
Awamu ya pili itafanyika baada ya wiki nne kutoka sasa.
Waliouawa wapindukia 41,000 Gaza na Ukingo wa Magharibi
Kampeni hii ya chanjo inaendelea kukiwa na kile kinachoitwa usitishaji wa mapigano kwenye vituo vinavyotolewa chanjo hiyo, katika wakati ambapo tayari mashambulizi ya Israel yameshauwa watu 40,819 kwenye Ukanda wa Gaza tangu tarehe 7 Oktoba.
Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa inasema wengi wa waliouawa ni wanawake na watoto.
Kwa upande mwengine, jeshi limeanza tena mashambulizi yake kwenye mji wa Tulkarem ulio kwenye Ukingo wa Magharibi. Matingatinga na magari ya kijeshi yameshuhudiwa kwenye mitaa ya mji huo wakati maduka yakiwa yamefungwa na wakaazi wengi kusalia majumbani mwao.
Soma zaidi: Mahakama ya Israel yataka wafanyakazi kusitisha mgomo mara moja
Uvamizi huu wa sasa, unaojumuisha uharibifu wa miundombinu, mashambulizi ya anga na vita vya mitaani, umejikita kwenye kambi za wakimbizi wa Jenin na Tulkarem, zilizo kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel.
Wizara ya Afya ya Palestina inasema watu 29, wakiwemo watoto watano, wameuawa tangu operesheni hiyo ianze wiki iliyopita.
Uvamizi huu wa Israel umezusha wasiwasi wa uwezekano wa vita vya Gaza kuhamia pia Ukingo wa Magharibi, ingawa Israel yenyewe inaiita hiyo kuwa ni operesheni ya kuzuwia mashambulizi dhidi ya raia wake.
Tangu Israel ianze mashambulizi yake kwenye Ukanda wa Gaza kufuatia uvamizi wa wanamgambo wa Kipalestina wa Oktoba 7, tayari watu 681 wameshauawa kwenye Ukingo wa Magharibi na wengine wapatao 5,700 kujeruhiwa.
Vyanzo: Reuters, AP