1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

WHO yaahidi tathmini huru kuhusu janga la covid-19

Admin.WagnerD18 Mei 2020

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema tathmini huru ya jinsi janga la kirusi cha corona linavyoshughulikia itaanzishwa haraka iwezekanavyo na China imeunga mkono hatua hiyo.

https://p.dw.com/p/3cQfa
Ukraine WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus
Picha: picture-alliance/dpa/P. Gonchar

Mkuu huyo wa WHO ametoa ahadi hiyo wakati wa mkutano wa wa baraza kuu la shirika hilo uliofanyika kwa njia ya kidijitali ambapo rais wa China, Xi Jinping aliitetea nchi yake kuhusu ilivyoushughulikia mgogoro huu.

Rais wa Marekani Donald Trump amehoji utendaji wa WHO wakati wa janga hili na kuongoza ukosoaji wa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu hatua zilizochukuliwa na China  kushughulikia suala hili katika kipindi cha mwanzoni kabisa cha mgogoro huu.

Aidha katika mkutano huo ulioratibiwa kutokea makao makuu ya WHO mjini Geneva, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa upande wake amesema nchi zinahitaji kushirikiana kulishinda janga hili na kwamba hakuna nchi inayoweza kulitatua tatizo hili peke yake.

Schweiz Genf WHO-Zentrale
Makao makuu wa shirika la WHO mjini Geneva, Uswisi.Picha: picture-alliance/imageBROKER/K. Petersen

Kadhalika wanachama wa shirika hilo wamekubaliana katika mkutano huo kuahirisha mjadala kuhusu kuipa nafasi Taiwan ya kuwa mwanachama muangalizi.Uamuzi huo umefikiwa licha ya Marekani na nchi nyingine kuzidisha shinikizo katika siku za karibuni kutaka Taiwan ikubaliwe.

Guterres asema covid-19 ni mwamko mpya

Akizungumza mwanzoni mwa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema janga la virusi vya corona ni fursa nzuri ya kuijenga upya dunia lakini akitilia shaka kujitolea kwa mataifa kutimiza lengo hilo.

Guterres ameongeza kuwa janga hilo limefichua udhaifu ulioko sio tu kwenye mifumo ya afya, lakini pia katika taasisi za kimataifa zinazoshughulikia mizozo ya hali ya hewa, usalama wa mitandao na kuondolewa kwa silaha za nyuklia.

Pia ameongeza kusema kuwa mataifa tofauti yamefuata njia tofauti na wakati mwingine kuchukuwa hatua zinazotiliwa shaka na kwamba mataifa yote yanakabiliwa na athari zake.

Guterres amesisitiza wito wake wa shirika la WHO kuongoza katika hatua za kimataifa za kukabiliana na janga hilo, kupanuliwa kwa huduma za afya za kiakili na sera za kushughulikia matatizo ya kijamii na kiuchumi yaliosababishwa na janga hilo.

Italien Milan - Krankenschwester
WHO imekosolewa na baadhi ya viongozi wa dunia kwa namna ilivyoshughulikia janga la virusi vya corona.Picha: Imago Images/Independent Photo Agency Int./M. Passaro

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa pia amethibitisha kuwa bara Afrika litatoa ''msaada kamili'' kwa shirika la WHO ambalo amesema limekuwa muhimu kuongoza katika mikakati ya kimataifa ya kukabiliana na janga la virusi vya corona.

Rais wa China, Xi Jinping, pia ameuambia mkutano huo kuwa nchi yake inaunga mkono ''ukadiriaji makhsusi'' wa jinsi dunia ilivyolishughulikia janga hilo baada ya kudhibitiwa kwake.

Xi amebainisha kuwa China ''imekuwa na mtazamo wazi na uwajibikaji'' na kutoa habari kuhusu virusi hivyo kwa wakati ufaao.

Chanzo: Mashirika