1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Visa vya Ebola nchini DRC vyaendelea kupungua

Saleh Mwanamilongo
12 Februari 2020

Kamati ya dharura ya wataalamu wa shirika la afya ulimwenguni imekutana siku ya Jumatano mjini Geneva na kuelezea ikiwa ugonjwa wa Ebola sio tena dharura ya kiafya kwa umma au hapana nchini DRC.

https://p.dw.com/p/3XgSu
WHO Generaldirektor Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus
Picha: Reuters/WHO/C. Black

Shirika la afya ulimwenguni, WHO, linatarajiwa kutangaza endapo ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo bado ni janga la umma kiafya ama la, licha ya tayari mkuu wa shirika hilo kusema kwamba ni lazima kuweko na tahadhari kwa sababu bado uwezekano wa maambukizi upo. Kuanzia wiki iliyopita hadi sasa, ni watu watatu tu walioripotiwa kuambukizwa. 

Kamati ya dharura ya wataalamu wa shirika la afya ulimwenguni imekutana Jumatano mjini Geneva. Kwenye mkutano wa Jumanne, kiongozi wa shirika la WHO, Tedros Adhom Ghebreyesus, alisema kwamba hali ya ugonjwa wa Ebola nchini Kongo imetia moyo lakini ni lazima kueko na tahadhari:

''Ingawa ulimwengu umeyapa kipaumbele ugonjwa wa virusi vya Corona, hatutakiwi kuisahau Ebola. Tumetiwa moyo zaidi na hali iliyoko hivi sasa. Tuna visa viattu pekee vya watu waliombukizwa Ebola toka wiki iliyopita na mnamo kipindi cha siku tatu hizi hakuna kisa hata kimoja'', amesema Tedros. 

Dokta Tedros ameongeza kwamba hali hiyo haimanishi kwamba ugonjwa wa Ebola umemalizika. Kisa chochote kipya kinaweza kuusambaza tena ugonjwa huo. Mkuu huyo anatarajiwa kuwasili mjini Kinshasa siku ya Alhamis, ambako atakutana na Rais Felix Tshisekedi ili kuzungumzia uwezekano wa kuboreshwa mfumo wa kiafya nchini Kongo.

Kongo Ein Kind bekommt eine Ebola-Impfung in Goma
Muuguzi akimpatia chanjo ya Ebola mtotoPicha: Getty Images/AFP/A. Wamenya

Ebola ilianzia wapi?

Ugonjwa wa Ebola uliozuka Agosti  2018 kwenye kijiji cha Mangina, mtaani Beni, Kivu ya Kaskazini, umeathiri pia maeneo kadhaa ya jimbo jirani la Ituri. Watu wapatao 2,300 wamekufa kutokana na Ebola.

Hatua ya kutangaza ikiwa ugonjwa huo ni dharura ya kiafya kwa umma ama la inatokana na bodi ya wataalamu wa kimataifa  wa shirika la WHO. Wataalamu hao hukutana kila baada ya miezi mitatu mara unapotangazwa ugonjwa.

Symbolbild Masernkrise
Mwathirika wa ugonjwa wa Ebola akizikwa eneo la Beni Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Julai mwaka uliopita, kamati hiyo ilitangaza Ebola kuwa dharura ya kiafya ya kimataifa kufuatia kugunduliwa kwa kisa kimoja cha mtu alieambukizwa na Ebola mjini Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu ya Kaskazini.

Vita dhidi ya Ebola huko mashariki mwa Kongo, vina changamoto za kipekee kutokana na na mashambulizi ya makundi ya wapiganaji. Licha ya matumizi ya aina mbili ya chanjo, ugonjwa wa Ebola unaendelea kwa zaidi ya miezi kumi na minane sasa kutokana na kile shirika la WHO kinaelezea kwamba ni baadhi ya raia kutoamini kuweko na ugonjwa huo, huku wengine wakikataa kupewa chanjo na vile vile kutotekeleza hatua za kimsingi za usafi.

Hii ni mara ya kumi sasa ugonjwa wa Ebola kuzuka nchini Kongo, lakini huu unaondelea ndio uliosababisha maafa makubwa zaidi.

 AFPE/ AFPF