1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Muafaka wa kuzuia magonjwa ya milipuko wahitajika

30 Novemba 2021

Shirika la Afya ulimwenguni WHO hapo jana lilifanya mkutano wenye lengo la kujadiliana kuhusu makubaliano ya kimataifa yanayohusiana na namna ya kuzuia majanga katika miaka ijayo

https://p.dw.com/p/43e6t
WHO-Chef | Tedros Adhanom Ghebreyesus
Picha: Fabrice Coffrini/REUTERS

Wakati wasiwasi ukiongezeka kuhusu aina ya kirusi cha Omicron, Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO limesema maamuzi yanayhokuliwa kwa hofu na viongozi wa ulimwengu yanaonyesha haja ya dharura ya kuwepo na muafaka wa kimataifa kuhusu magonjwa ya milipuko.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa siku tatu wa Afya Ulimwenguni jijini Geneva, Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kuibuka kwa aina ya kirusi kilichobadilika pakubwa cha Omicron kunadhihirisha ni jinsi hali yetu ilivyo hatarini.

Alisema wanasayansi kote ulimwenguni wanafanya kazi kwa haraka kubaini kama kirusi cha omicron, kilichogunduliwa kwa mara ya kwanza Afrika Kusini, kinaambukiza Zaidi au kama chanjo zinafanya kazi dhidi yake.

Australien Covid-19 | Reisebeschränkungen wegen der Omikron-Variante
Wasafiri lazima wafanyiwe vipimo vya COVID-19 Picha: Loren Elliott/REUTERS

Mkuu huyo wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, hata hivyo amesisitiza kuwa Mkutano wa Afya Ulimwenguni wenye nchi wanachama 194 unahitaji kuhakikisha kuwa msingi unawekwa kwa ajili ya kupatikana muafaka unaoweza kuzuia magonjwa ya milipuko katika siku za usoni.

Tedros amesema hatupaswi kuwa na tukio jingine la kutufanya tuamke. 

Soma pia: WHO: Huenda kirusi cha Omicron kikasambaa kote duniani

Mbona WHO imetaja omicron kuwa ‘kitisho kikubwa'?

Mapema Jumatatu, WHO ilitoa tarifa ya tathmini yake ya karibuni ya kirusi cha omicron – ikikitaja kuwa kinaleta kitisho kikubwa sana cha ongezeko la maambukizi ulimwenguni. Wakati ikisubiriwa kuona kama kirusi hicho kinaongeza kitisho cha ugonjwa mbaya sana au kifo – kubadilika mara kadhaa katika siku za nyuma kumesababisha kitisho kikubwa cha maambukizi ya kujirudia katika wagonjwa ambao tayari wamepona kutokana na COVID.

Infografik COVID-19 Länder mit Omikron 29.11. 11:20 EN

Taarifa ya WHO imesema kwa kulingana na sifa hizi, huenda kukawa na ongezeko la visa vya COVID-19 katika siku za usoni, ambalo huenda na madhara makubwa, kulingana na sababu kadhaa ikiwemo ni wapi ongezeko hilo linatokea.

Ni uungwaji mkono kiasi gani uliopo kwa muafaka wa janga?

Viongozi kutoka Ujerumani na Umoja wa Ulaya wameunga mkono muafaka wa kimataifa wa majanga ya kiafya, wakitoa wito wa ufadhili thabiti kwa WHO.

Kaimu Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alipendekeza nchi wanachama kuongeza michango yao kwa kiasi kikubwa – kumaanisha hadi asilimia 50.

Soma pia: Ujerumani, Uingereza na Italia zathibitisha visa vya Omicron

Kansela huyo anayeondoka pia aliunga mkono juhudi za kuufanya muafaka wa kuzuia majanga ya kiafya kuwa wa kisheria – ambao kwa sasa haupo kwenye meza katika makubaliano ya rasimu.

Merkel anatarajiwa kufanya leo mazungumzo ya video na magavana wa majimbo ya Ujerumani kujadili ongezeko kubwa la visa vya virusi vya corona kote nchini.

Mawaziri wa afya kutoka kundi la nchi saba tajiri ulimwenguni la G7 wamesema kuna uungwaji mkono imara wa kuundwa mtandao wa kimataifa wa kufuatilia kirusi hicho ndani ya mfumo wa Shirika la Afya Ulimwenguni.

USA COVID-19 | PK Biden zu Omikron
Biden asema omicron haipaswi kusababisha hofuPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Katika taarifa ya pamoja baada ya mkutano wao wa video, walisifu kazi nzuri kabisa iliyofanywa na Afrika Kusini katika kugundua kirusi hicho na kuwafahamisha wengine kukihusu.

Marekani imekuwa ikisita kukubali kusaini mkataba unaofungamanisha kisheria, lakini ikafikia makubaliano na mataifa mengine wanachama kuanzisha mchakato wa kupata muafaka wa kimataifa.

Nini kipo kwenye rasimu hiyo?

Rasimu hiyo, ambayo inatarajiwa kuidhinishwa mwishoni mwa mazungumzo ya WHO kesho Jumatano, inaweka hatua za muda mrefu.

Nchi zimekubali kwa muda kuanzisha chombo cha kati ya serikali mbalimbali ambacho kitatayarisha na kuujadili muafaka huo. Muafaka wenyewe utaangazia maeneo matatu: kuzuia janga, kujiandaa na kulishughulikia janga.

Soma pia: Kirusi cha Omicron chazusha taharuki ulimwenguni

Mkataba, au aina nyingine ya makubaliano huenda yasiwe tayari kwa miaka kadhaa. Muda wa mwisho uliowekwa kwa sasa ni mwaka wa 2024.

rs/wmr (dpa, AFP)