WHO: Janga la Ebola halipo tena
14 Januari 2016Mlipuko huo mkubwa wa Ebola kuwahi kushuhudiwa katika historia ulivuruga uchumi na mifumo ya afya katika nchi tatu zilizoathirika kwa kiasi kikubwa katika eneo la Afrika Magharibi baada ya kuzuka kusini mwa Guinea mnamo Desemba 2013.
Katika kilele chake, Ebola ilisambaa nchini Guinea, Liberia na Sierra Leone, huku miili ikitapakaa mitaani na hospitali zikifurika wagonjwa kutokana na mamia ya visa vipya vya maambukizi ya virusi hivyo kila wiki. Rick Brennan, mkuu wa Shirika la Afya Duniani – WHO anayehusika na misaada ya kiutu amesifu mafanikio hayo lakini akasema “kazi bado haijakwisha kabisa”. "WHO inawapongeza watu, serikali na wahudumu wa afya katika Afrika Magharibi katika juhudi hii kubwa. Huu umekuwa mlipuko mkubwa wa virusi vya Ebola na uliochukua mda mrefu. Kumekuwa na visa 28,000, karibu vifo 11,300 na hii ilihitaji juhudi kubwa ya pamoja".
Kumekuwa na mchanganyiko wa maoni ya wenyeji wa Monrovia ambao wengine wao wanasema kuwa wamezoea kusikia habari nzuri zikitangazwa kuhusu ugonjwa huo na kisha kufuatwa na visa vipya vya maambukizi.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameonya kuwa eneo hilo la Afrika magharibi linaweza kutarajia matukio ya hapa na pale katika mwaka ujao lakini akaongeza kuwa tunatarajia kuona uwezekano na viwango vya visa hivyo vikipungua baada ya muda.
Daktari Peter Graaff ni mkurugenzi mkuu wa kitengo cha WHO cha kupambana na Ebola "Tunahitaji kuendelea kushirikiana, kabla ya mlipuko wa Ebola, nchi tatu za Afrika magharibi zilikuwa na raslimali chache, hazikupata msaada wa kutosha wa kiufundi wa kuiwezesha sekta ya kiafya. Tutatumia ujuzi tuliopata katika kukabiliana na Ebola ili kuwa waangalifu zaidi na kuweza kuyashughulikia matatizo yoyote yatakayotukumba katika siku za usoni"
Athari za kiuchumi zilizotokana na janga hilo bado zinaonekana. Benki kuu ya Dunia inakadiria kuwa uharibu wa kiuchumi kutokana na mipuko huo ambao uliathiri kabisa sekta za madini, kilimo na utalii nchini Liberia, Sierra Leone na Guinea ni dola bilioni 2.2 katika mwaka wa 2014-2015.
Mkurugenzi mkuu wa WHO Margaret Chan ameitaja miezi mitatu ijayo kuwa “muhimu zaidi” wakati mashirika ya kigeni ya matibabu yakifunga shughuli zake katika eneo la Afrika Magharibi na wizara za afya katika nchi hizo kuchukua usukani.
Umoja wa Ulaya, kwa pamoja na michango kutoka kwa mataifa binafsi wanachama, zilichangisha karibu euro bilioni 2 kwa ajili ya kuushughulikia ugonjwa huo, na umesema sasa utaachana na msaada wa dharura na badala yake kuangazia maendeleo ya mataifa yaliyoathirika
Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Yusuf Saumu