WFP: Mamilioni wakabiliwa na kitisho cha njaa Haiti
13 Machi 2024Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula - WFP, amesema watu milioni nne wanakabiliwa na kitisho kikubwa cha njaa kutokana na ukosefu wa usalama wa chakula nchini Haiti.
Waziri Mkuu wa Haiti kuondoka Ijumaa
Watu milioni moja miongoni mwao wanakaribia kabisa kutumbukia kwenye janga la njaa nchini humo kutokana na kuongezeka hivi karibuni kwa machafuko yanayosababishwa na magenge ya uhalifu.
Jean-Martin Bauer mkurugenzi wa shirika la WFP katika mkutano na waandishi habari kwa njia ya mtandao amesema hali imezidi kuwa mbaya na watu 15,000 wameachwa bila makaazi katika kipindi cha mwishoni mwa wiki ya mwanzo tu ya mwezi huu wa Machi katika mji mkuu Port-Au-Prince.
Kwa ujumla watu walioachwa bila makaazi nchini humo wamefikia 360,000 na Umoja wa Mataifa unasema nusu ya watu hao ni watoto. Mkurugenzi huyo wa WFP, Jean-Martin Bauer amesema chakula katika ghala lake nchini Haiti kitamalizika ndani ya wiki chache zijazo ikiwa bandari haitofunguliwa tena kwa ajili ya kuingiza mahitaji.