Ziara ya Westerwelle nchini China
15 Januari 2010Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, alieanza ziara nchini China leo , amefanya mazungumzo na waziri mwenzake juu ya masuala ya haki za binadamu vilevile.
Waziri Westerwelle amesema masuala ya uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kutoa maoni ni sehemu ya msingi wa sera za nje za Ujerumani.
Waziri Westerwelle anaefanya ziara ya China kwa mara ya kwanza tokea ashike wadhifa wa waziri wa mambo ya nje ameashiria uwezekano wa kukutana na kiongozi wa kidini anaepigania uhuru wa Tibet, Dalai Lama . Waziri Westerwelle ambae leo alikutana na waziri mkuu wa China Wen Jiabao, amesema kwamba tayari ameshawahi kuwa na fursa ya kukutana na Dalai Lama mnamo siku za nyuma.
Hata hivyo, ameeleza kwamba kwa sasa hakuna mkutano uliopangwa kufanyika baina yake na kiongozi huyo wa kidini.
Waziri Westerwelle na waziri mwenzake, Yang Jiechi, walifanya mazungumzo na walipeana mawazo juu ya suala la Tibet. Waziri Yang alimwambia mgeni wake kutoka Ujerumani kwamba China inapinga mawasiliano yote baina ya Dalai Lama na viongozi wa nchi za nje. Mawaziri hao pia walijadili suala la Iran. China imesisitiza kwamba yapo masuala muhimu sana, lakini China inataka kuletwa suluhisho kwa njia ya mazungumzo.
Kwa upande wake, waziri Westerwelle amesema mipango yoyote ya Iran ya kuunda silaha za nyuklia haitakubalika na kwamba Ujerumani ipo tayari kuiwekea nchi hiyo vikwazo zaidi ikiwa mazungumzo yanayofanyika sasa yatashindikana.
Mwandishi/Mtullya Abdu/ ZA AFP.
Mhariri: Miraji Othman