1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa nje wa Marekani Pompeo akutana na Lavrov wa Urusi

Oumilkheir Hamidou
14 Mei 2019

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Sergei Lavrov amemwambia waziri mwenzake wa Marekani Mike Pompeo, "wakati umewadia kwa Moscow na Washington kuweka kando miaka kadhaa ya uhasama na kubuni njia ya kushirikiana".

https://p.dw.com/p/3IUL6
Russland Minister Lavrov and US Secretary of State Pompeo
Picha: picture-alliance/dpa/A. Novoderezhkin

Mike Pompeo yuko ziarani katika mji unaopakana na bahari nyeusi wa Sochi kwa mazungumzo pamoja na waziri mwenzake wa Urusi na baadae amepangiwa pia kukutana na rais Vladimir Putin.

Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeingia sumu kutokana na madai-yaliyokanushwa na Moscow-kwamba Urusi imejaribu kushawishi matokeo ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2016, na pia kutokana na tofauti zao za maoni katika mzozo wa Venezuela, Iran, Syria na Ukraine.

"Tunaona kuna shaka na chuki" amesema Lavrov mwanzoni mwa mazungumzo yake pamoja na Pompeo."Hali hii inakorofisha usalama wa nchi yetu na nchi yenu pia na kusababisha wasi wasi ulimwenguni.Tunahisi wakati umewadia wa kubuni uhusiano mpya wenye manaufaa wa zaidi kwa pande zote" amesisitiza waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Lavrov na kuongeza tunanukuu"Tuko tayari ikiwa wenzetu wa Marekani wako tayari pia."

Ziara ya Mike Pompeo ni hatua ya mwanzo ya mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya Moscow na Washington tangu mwendesha mashitaka mkuu wa Marekani Robert Muller alipowasilisha ripoti yake iliyotathmini nafasi iliyoshikiliwa na Urusi katika uchaguzi wa rais mwaka 2016 nchini Marekani.

Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la nishati ya nuklea
Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la nishati ya nukleaPicha: picture-alliance/dpa/H.Punz

Mzozo wa nuklea wa Iran itakuwa mojawapo ya mada mazungumzoni

Akijibu matamshi ya Lavrov ,Mike Pompeo amesema amekuja Sochi kwasababu rais Trump amedhamiria kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili."Tuna tofauti zetu na kila nchi itatetea masilahi yake na kupigania masilahi ya wananchi wake" amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani. Hata hivyo anasema Marekani na Urusi hawahasimiana kwa kila kitu akikumbusha maarifa yake binafsi katika juhudi za kupambana na ugaidi pamoja na Urusi ambazo anasema zimeokoa maisha ya wamarekani na warusi pia."

Mazungumzo ya leo usiku kati ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani na rais Vladimir Putin wa Urusi yatagusia masuala ya kimataifa ikiwa ni pamoja na kudhibitiwa silaha za nuklea na hasa kwa kuzingatia Iran na Korea ya kaskazini, mzozo wa Venezuela na Syria.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa

Mhariri: Sekione Kitojo