1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa fedha aliyefutwa Afrika Kusini azungumza

31 Machi 2017

Aliyekuwa waziri wa fedha  wa Afrika Kusini, Pravin Gordhan amezungumza na waandishi habari na kusema amechoshwa kusikia kwamba alifanya mikutano ya siri kuihujumu serikali.

https://p.dw.com/p/2aTIL
Südafrika Kapstadt Finanzminister Pravin Gordhan
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Hutchings

Kufutwa kazi kwa Gordhan anayeheshimika na kutajwa kuwa ni mchapakazi na muadilifu, kumesababisha hasira dhidi ya rais Jacob Zuma hata kutoka kwa vigogo wa ndani ya chama cha ANC, akiwemo Makamu wa rais Cyril Ramaphosa. 

Zuma amemteua, Malusi Gigaba ambaye alikuwa waziri wa mambo ya ndani kuchukua nafasi ya Gordhan. Gigaba ni mfuasi mzuri wa Zuma na ambaye mara zote amekuwa tayari kumtetea Rais Zuma licha ya kwamba rais huyo anakabiliwa na tuhuma lukuki za ufisadi na ongezeko la mashitaka ya kisheria.

Südafrika | Präsident Jacob Zuma
Rais Jacob Zuma amekosolewa vikaliPicha: REUTERS/S. Hisham

Alipata ukosoaji mkubwa baada ya kuanzisha sheria ngumu ya upatikanaji wa viza ya kuingia nchini humo, hatua iliyoathiria kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii, na ambaye pia ana uzoefu mdogo kuhusu masuala ya uchumi.

Raia wengi nchini Afrika Kusini walimchukulia Gordhan kama mlinzi bora wa uchumi ambao hadhi yake ya viwango inaweza kushushwa kabisa na taasisi za kimataifa zinazotoa makadirio ya mikopo katika siku chache zijazo. Kutimuliwa kwa Gordhan ni pigo jingine kwa nchi hiyo iliyostawi zaidi kiviwanda Barani Afrika, ambayo uchumi wake ulikua kwa asilimia 0.5 tu mwaka jana, na kukabiliwa na mzozo wa ukosefu wa ajira kwa asilimia 27. 

Mamia ya waandamanaji walikusanyika nje ya ofisi za wizara ya fedha ambako Gordhan aliwaambia waandishi wa habari kwamba inamchosha kusikia akituhumiwa kwa kuendesha mikutano ya siri inayolenga kuidhoofisha serikali.

Makamu wa rais, Cyril Ramaphosa ambaye anaonekana kama mgombea anayeweza kuchukua madaraka kutoka kwa Zuma kama kiongozi wa chama tawala, kwenye mkutano wake mnamo mwezi Desemba aliita hatua ya kumtimua Gorharn kuwa isoyokubalika.

Südafrika Richter Mogoeng Mogoeng in Pretoria
Makamu wa rais, Cyril Ramaphosa amemkosoa ZumaPicha: picture alliance/AA/S. Seshibedi

Hatua hiyo ya rais Zuma kumtimua Gordhan imechochea mpasuko ndani ya chama kikongwe cha ANC, huku upinzani ukiapa kupinga hatua hiyo mahakamani. Gordhan ni miongoni mwa mawaziri 10 waliopitiwa na mabadiliko kwenye baraza la mawaziri lenye idadi jumla ya mawaziri 35, yaliyofanywa na rais Zuma na mawaziri wapya wameapishwa leo hii.

Mabadiliko haya ya baraza, yanakuja wakati kukiongezeka kwa miito ya Zuma kuachia ngazi. "Ni bunge ndio lilimpa kazi Zuma, na ni bunge ndilo linaweza kumfuta kazi", amesema kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance Mmusi Maimane, ambae alisema jana kuwa chama chake kitazindua mchakato wa kura ya kutokuwa na imani na Rais. 

Mwandishi: Lilian Mtono.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman