1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mpya wa Marekani Pompeo ziarani Mashariki ya Kati

28 Aprili 2018

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo anafanya ziara muhimu kwa nchi washirika wa Marekani katika kanda ya Mashariki ya Kati. Ameanza ziara hiyo kwa kutoa ahadi ya kurejesha mahuasiano mazuri ya kidiplomasia.

https://p.dw.com/p/2wqtr
Nato Außenminister Treffen in Brüssel Mike Pompeo
Picha: picture-alliance/dpa/V. Mayo

Baada ya kuhudhuria mazungumzo ya Jumuiya ya kujihami ya nchi za magharibi NATO mjini Brussels, Pompeo anatarajia kuanza ziara ya siku tatu katika nchi za Saudi Arabia, Israel na Jordan ili kuwasilisha mipango ya Rais Donald Trump kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani Pompeo amesisitiza kwamba rais Trump bado hajafanya uamuzi, hata ingawa inategemewa anatarajiwa kuiondoa Marekani katika mkataba huo mwezi ujao, na kuweka tena vikwazo dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran.

Waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo
Waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani Mike PompeoPicha: Reuters/Y. Herman

Waziri huyo ambaye zamani alikuwa mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Marekani CIA, aliapishwa kama mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Trump mnamo siku ya Alhamis na kisha kuelekea mjini Brussels baada ya masaa mawili amesema atashauriana na wapinzani wa Iran katika kanda ya Mashariki ya Kati kabla ya rais Trump kutoa tangazo rasmi.

Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson
Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani Rex TillersonPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Harnik

Waziri huyo mpya wa mambo ya nje amesema binafsi, anataka kuzionesha nchi za nje pamoja na wenzake kwamba diplomasia ya Marekani imerudi upya baada ya uongozi wa wasiwasi wa mtangulizi wake aliyeachishwa kazi bwana Rex Tillerson. Pompeo ameahidi pia kuzungumza na wafanyakazi wa wizara ya mambo ya nje atakaporejea Marekani Jumanne ijayo.

Muda mfupi baada ya kuthibitishwa wakosoaji wamemkosoa bwana Pompeo kwa matamshi yake ya awali dhidi ya Uislamu na pia ndoa za jinsia moja, ambapo wamesema hakuzingatia maadili ya sera za nje za Marekani.

Lakini pia kuna matumaini, katika baadhi ya maafisa wanao andamana naye katika safari hii, kwamba diplomasia ya Marekani sasa imepata mkuu ambaye ataweza kuzungumza kwa niaba ya rais Donald Trump na kuzingatia mipango ya msingi wa wizara ya mambo ya nje.

Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Adel bin Ahmed Al-Jubei
Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Adel bin Ahmed Al-JubeirPicha: Reuters/H. I. Mohammed

Nchini Saudi Arabia Jumamosi hii, Pompeo atafanya mazungumzo na mwenzake wa Saudi Arabia Adel al-Jubeir katika jiji la Riyadh, na baadae atakula chakula cha jioni na mwana Mfalme Mohammed bin Salman.

Bin Salman maarufu kama MBS, ndiye mrithi wa mfalme na muanzilishi wa mabadiliko ya kijamii nchini Saudi Arabia na aliyeanzisha mapambano dhidi ya rushwa ili kuwadhibiti wana familia ya kifalme katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Kama Trump na Pompeo, mpinzani mkubwa wa Iran, lakini vita anavyoviunga mkono dhidi ya wanamgambo wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran huko nchini Yemen havina mafanikio na vimechangia maafa makubwa ya kibinadamu nchini humo.

Kushoto: Mwana mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman Kualia rais wa Marekani Donald Trump
Kushoto: Mwana mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman Kualia rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/JE. Vucci

Rais Trump pia anaitaka Saudi Arabia kuongeza bidii na kuongeza fedha kwa ajili ya kuunga mkono operesheni inayoongozwa na Marekani nchini Syria dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislam ili kuyawezesha majeshi ya Marekani kurudi nyumbani haraka zaidi.

Baada ya ziara ya Saudi Arabia, Pompeo atakwenda Israel kwa ajili ya kufanya mazungumzo na mshirika wa Marekani, Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na kisha atazuru Jordan nchi rafiki wa Marekani iliyo na mpaka mrefu baina yake na Syria ambayo inakumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi:Zainab Aziz/AFPE

Mhariri:Sylvia Mwehozi