1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Pakistan azuru Kashmir

14 Agosti 2019

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan ameitumian sherehe za Siku Kuu ya Uhuru kuikosoa India kwa hatua ilizochukua katika jimbo linalogombaniwa la Kashmir

https://p.dw.com/p/3NsN2
China Pakistans Premierminister Imran Khan
Picha: AFP/T. Peter

Pakistan imeadhimisha leo miaka 73 ya Uhuru wake, huku viongozi wa serikali hiyo wakitumia hotuba zao kuikosoa India kutokana na vitendo vyake katika jimbo la Kashmir, ambalo linagombaniwa na nchi zote mbili. Rais Arif Alvi amehutubia katika sherehe hizo akisisitiza uungwaji mkono kwa watu wa Kashmir hadi watakapopata haki ya kujitawala wenyewe.

Naye Waziri Mkuu Imran Khan amesema katika taarifa kuwa Siku Kuu ya Uhuru ni fursa ya kuwa na furaha lakini leo ni siku ya huzuni unatokana na shida wanayopitia ndugu zao wa Kashmir katika majimbo yanayokaliwa ya Jammu na Kashmir ambao ni wahanga wa uchokozi wa India. Khan ameapa kusimama na watu wa Kashmir.

India inatawala Bonde la Kashmir lenye idadi kubwa ya watu na jimbo lenye Wahindu wengi karibu na mji wa Jammu, wakati Pakistan inadhibiti sehemu ya mpaka wa upande wa magharibi inayofahamika kama Azad Kashmir. China ina kipande chenye idadi ndogo ya watu katika eneo la nyanda za juu la kaskazini.

Indien Kaschmir Opferfest
Usalama katika jimbo la Jammu umeimarishwaPicha: picture-alliance/AP Photo/C. Anand

Serikali ya New Delhi iliifuta hadhi maalum ya sehemu yake ya Kashmir ya Himalaya inayofahamika kama Jammu na jimbo la Kashmir, mnamo Agosti 5 na kuchukua hatua ya kutuliza ghasia kwa kukata mawasiliano na kuweka vizuizi kwa uhuru wa watu kutembea.

Hatua ya India kufuta hadhi maalum ya majimbo ya Jammu na Kashmir yanazuia haki yao ya kutunga sheria zao na kuwaruhusu watu wasio wakaazi kununua mali.

Serikali ya Waziri Mkuu wa India Narendra Modi imesema sheria za zamani zinazowazuia watu kutoka nje ya Kashmir kununua mali, kuhamia huko na kupewa kazi za serikali ziliathiri maendeleo

Pakistan ilijibu kwa kusitisha mikataba ya kibiashara ya pande mbili na njia zote za usafiri na India, pamoja na kumtimua balozi wa India mjini Islamabad.

Wakati huo huo, Gavana wa Kashmir Satya Pal Malik amesema vikwazo vya kusafiri katika jimbo hilo vitaondolewa kesho Alhamisi baada ya sherehe za leo za Siku Kuu ya Uhuru. Ijapokuwa amesema mawasiliano ya simu na mtandao wa intaneti vitaendelea kufungwa.

Maelfu ya wanajeshi wa India wamewekwa katika mji mkuu wa jimbo hilo Srinagar na miji mingine na vijiji.

Huku hayo yakijiri, Pakistan imeutaka Umoja wa Mataifa kuitisha kikao cha dharura cha Baraza lake la Usalama kuhusiana na mzozo huo wa Kashmir.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Pakistan Shah Mehmood Qureshi amesema katika barua kwa Baraza la Usalama kuwa hali ya sasa inaweka kitisho kikubwa kwa amani na usalama wa kimataifa.