1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mohammad al-Bashir aahidi kutenda haki kwa raia wote

Angela Mdungu
11 Desemba 2024

Waziri Mkuu mpya wa Syria Mohammad al-Bashir amesema Muungano wa makundi yenye misimamo mikali ya Kiislamu yaliyomuondoa mamlakani Rais Bashar al- Assad yatahakikisha kuwa yanatenda haki kwa makundi ya dini zote.

https://p.dw.com/p/4o1Ar
Serikali ya mpito Syria
Waziri Mkuu wa mpito wa Syria Mohammad al-BashirPicha: AL ARABIYA TV/Handout/REUTERS

Waziri Mkuu wa mpito wa Syria aliyeteuliwa Jumanne  amesema kuwa uongozi wake utahakikisha makundi yote ya raia nchini humo yanapata haki sawa.

Katika mahojiano yake na gazeti la Corriere della Sera, lililochapishwa Jumatano, Bashir pia amesema kwa sasa Syria ni taifa huru lenye heshima na utu hivyo anatoa wito kwa Wasyria wote waliokimbia vita kurudi nyumbani.

Mohammad al-Bashir amesema pia kuwa anakusudia kuwalinda raia wote na kuwapa huduma za msingi ingawa kulijenga upya taifa hilo kutakuwa kibarua kigumu kutokana na kukosa kuungwa mkono na mataifa ya kigeni.

Soma zaidi:Waziri mkuu wa Syria akiri, nchi yake haina fedha za kigeni

Al Bashir ameyazungumza hayo wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akisema kuwa anawaamini watu wa Syria katika kuchagua kinachowafaa kwa mustakabali wa taifa lao.

Katika hatua nyingine, wapiganaji wa makundi ya upinzani ya Syria wakiongozwa na kundi la Hayat Tahrir al-Sham lililomuondoa rais Assad madarakani wamepata udhibiti kamili wa mji mkubwa wa upande wa mashariki wa Deir al Zour kutoka mikononi mwa vikosi vya SDF vinavyoongozwa na wapiganaji wa Kikurdi.  Hayo ni kwa mujibu wa shirika la Syria linalofuatilia  haki za binadamu.

Vikosi vya SDF viko katika vijiji kadhaa mashariki mwa mto Euphrates ambavyo vilikuwa chini ya wanamgambo waliomuunga mkono Assad wanaosaidiwa na Iran.

Urusi: Tunafanya mawasiliano na utawala wa sasa wa Syria

Wakati huohuo, Ikulu ya Urusi, Kremlin imesema inafanya mawasiliano na uongozi mpya wa Syria kuhusu kambi zake za jeshi na wanajeshi walioko Syria.

Dimitry Peskov
Msemaji wa Kremlin, Dimitry Peskov Picha: Mikhail Tereshchenko/TASS/dpa/picture alliance

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano msemaji wa Kremlin Dimitry Peskov amesema, "Bila shaka tunafuatilia kwa karibu kinachoendelea Syria. Tunafanya mawasiliano na wanaodhibiti hali Syria. Ni muhimu kwa sababu kambi zetu za kijeshi na ubalozi wetu uko huko. Na pia suala linalohusu usalama wa maeneo hayo ni muhimu sana. Tutaendelea kufuatilia kwa karibu na kuendana na hali halisi inavyoendelea huko."

Kwingineko, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken anaelekea Mashariki ya Kati katika ziara yake ya 12 tangu mzozo wa Israel na Hamas ulipoibuka mwaka uliopita.

Ziara hiyo ni ya kwanza tangu utawala wa Bashar al Assad ulipoanguka Syria na kuzua hofu mpya ya kiusalama katika ukanda huo unaofukuta kwa mizozo.

Atakuwa Jordan na Uturuki Alhamisi na Ijumaa kwa mazungumzo yatakayojikita zaidi Syria, na kugusia matumaini ya makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.