1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wazimbabwe wasubiri matokeo ya uchaguzi kwa amani

31 Julai 2018

Kura zinaendelea kuhesabiwa nchini Zimbabwe na wananchi wanangoja matokeo kufuatia uchaguzi mkuu wenye ushindani mkali zaidi kati ya chama tawala na upinzani, huku kila upande ukijitabiria ushindi mkubwa.

https://p.dw.com/p/32MkN
Simbawe Präsidentschaftswahlen Wähler
Picha: Reuters/S. Sibeko

Kila mmoja kati ya Rais Emmerson Mnangagwa na mpinzani wake mkuu, Nelson Chamisa, alisema siku ya Jumanne (31 Julai) ana uhakika wa ushindi, baada ya uchaguzi huo wa kwanza tangu kumalizika kwa takribani miongo minne ya utawala wa Robert Mugabe.

Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 75 na ambaye alikuwa mkuu wa ujasusi na kisha msaidizi wa Mugabe wa muda mrefu kabla hajachukuwa madaraka kufuatia hatua ya jeshi kumuondoa kwa nguvu Mugabe mwezi Novemba, alisema alikuwa akipokea "taarifa nzuri sana" kutoka vyumba vya kuhesabu kura.

Naye Chamisa anayeongoza chama cha upinzani cha MDC alisema chama chake kimefanya vyema zaidi ya kilivyotegemea.

Wanadiplomasia wa Kimagharibi na waangalizi wa ndani walisema uchaguzi wa mara hii, ambapo asilimia 75 ya wapigakura walijitokeza, una ushindani mkubwa mno kiasi cha kutokuwa rahisi kutabiri mshindi wa moja kwa moja.

Tume ya uchaguzi ilisema shughuli ya kuhesabu kura inakwenda kwa utaratibu mzuri na chini ya usimamizi wa mawakala wa wagombea, vyama, na hata waangalizi wa kimataifa.

"Shughuli ya kuhesabu kura imeanza katika baadhi ya maeneo kwa mujibu wa sheria. Kura zinahisabiwa mbele ya waangalizi na waandishi wa habari walioko kwenye vituo va kuhesabia kura," Priscillah Cigumba, mwenyekiti wa tume hiyo, aliwaambia waandishi wa habari mjini Harare.

Umuhimu wa uchaguzi huu kwa Zimbabwe 

Simbabwe Wahl Robert Mugabe
Robert Mugabe akipiga kura yake kwenye uchaguzi wa tarehe 30 Julai 2018, wa kwanza kabisa kufanyika bila ya yeye kugombea.Picha: Reuters/S. Sibeko

Kufanya uchaguzi wa amani unaokubalika kuwa wa haki ndani na nje ni hatua muhimu sana kwa Zimbabwe kwa sasa, ambayo inaweza kulipunguzia taifa hilo la kusini mwa Afrika vikwazo vya kiuchumi na kuirejeshea ufadhili na uwekezaji wa kimataifa, unaohitajika sana kulizuwia lisiporomoke kabisa kiuchumi.

Yeyote atakayetangazwa mshindi anakabiliwa na jukumu kubwa la kuirejesha Zimbabwe kwenye mstari baada ya miaka 37 ya Mugabe kuiweka nchi hiyo kwenye kilele cha ufisadi, utawala mbaya na kutengwa kimataifa, mambo ambayo yameligeuza taifa lililowahi kuwa kigezo cha uchumi imara barani Afrika kutumbukia kwenye ufukara.

Hata hivyo, matokeo yoyote yawayo, bado kuna wasiwasi wa kuzuka machafuko. Ikiwa MDC itapoteza tena na kupinga matokeo, kunaweza kukafanyika maandamano yanayoweza kugeuka ghasia na hatua kali za kisheria ambazo zitazidi kuyakwamisha mageuzi ya kiuchumi. 

Na kama Mnangagwa atashindwa, Wazimbabwe wengi wanahofia kuwa baadhi ya makada wa chama tawala hawatakubali, hasa inapozingatiwa bahati nasibu waliyocheza kwa kumuondoa Mugabe.

Kwa mujibu wa sheria, tume ya uchaguzi ina siku tano za kukamilisha kutangaza matokeo ya uchaguzi huu, tangu siku kura zilipopigwa, ikimaanisha kuwa kufikia mwishoni mwa wiki, mshindi atakuwa amefahamika.

Chaguzi kadhaa chini ya Mugabe zilishuhudia ghasia, wizi wa kura na udanganyifu ambao ulikisaidia chama tawala (ZANU-PF) kuendelea kusalia madarakani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga