1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPakistan

Watu zaidi ya 57 wauwawa katika shambulio baya Pakistan

29 Septemba 2023

Maafisa nchini Pakistan wamesema zaidi ya watu 57 wameuwawa na wengine wengi wamejeruhiwa katika mkoa wa Balochistan, kufuatia mshambuliaji wa kujitoa muhanga kujilipua katika sherehe za kidini.

https://p.dw.com/p/4Wysg
Pakistan Anschlag in Quetta
Raia wa pakistan wakionekana nje ya hospitali kulikopelekwa waathiriwa wa shambulio la kujitolea muhanga BalochistanPicha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Maafisa wa usalama wamesema katika mkoa wa kusini magharibi wa Baluchistan, mshambuliaji wa kujitolea muhanga alijiripua wakati waumini walipokuwa wamekusanyika pamoja katika eneo la Mastung kilomita 40 kusini mwa mji wa Quetta.

Hazoor Bakhsh aliye na miaka 49 na aliyeshuhudia kisa hicho, anasema wakati wa tukio miguu yake ilitetemeka na akajikuta ameanguka chini na baadae kuwaona watu wengi wametapakaa kila mahali, huku wengine wakiitisha usaidizi.

Serikali ya eneo hilo ilitumia mara moja mitandao ya kijamii kuomba watu kuchangia damu ya kuwaokoa waathiriwa wa mkasa huo, waliokimbizwa katika hospitali zilizokuwa karibu.

Munir Ahmed Shaikh, naibu mkuu wa polisi wa mkoa wa Balochistan amesema idadi ya waliokufa kwa sasa wanafikia 57, lakini kuna hofu ya idadi hiyo kupanda. Takriban watu 70 ndio waliojeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea mchana wa leo.

Shambulio hili limetokea wakati Pakistan ikijitayarisha kuandaa uchaguzi mkuu mwezi Januari mwaka ujao, huku ikipambana na mgogoro wa kisiasa, uchumi mbaya, na kushamiri kwa mashambulio ya wanamgambo, yaliopamba moto baada ya kundi la Taliban kurejea madarakani mwaka 2021 nchini Afghanistan.

Serikali imetangaza siku tatu za maombolezo

Pakistan Anschlag in Quetta
Watu waliojeruhiwa katika shambulio la Pakistan wapokea matibabu katika moja ya hospitali nchini humoPicha: District Police Office/AP Photo/picture alliance

Wakati kusherehekewa kwa siku ya kuzaliwa ya Mtume Mohammed kwa waumini wa Kiislamu ikiridhiwa kwa madhehebu yote ya Kiislamu nchini Pakistan na katika maeneo mengine ya Waislamu duniani, baadhi yao wanaliona hilo kama kitu kilichobuniwa.

Waziri wa habari wa Balochistan Jan Achakzai, ametangaza siku tatu za maombolezo kufuatia shambulio hilo. Balochistan mkoa ulio na watu wachache ni ngome ya makundi kadhaa ya wanamgambo wanaopigania kile wanachokiita uhuru au kugawana kwa usawa rasilimali ya eneo hilo.

Katika tukio jengine, mshambuliaji pia wa kujitoa alijiripua ndani ya msikiti mmoja mkoani Khyber Pakhtunkhwa na kusababisha paa la jumba hilo kuanguka na kuwauwa watu wanne.

Wanaume wawili waliokuwa wamevalia vesti za vilipuzi walijaribu kujipenyeza msikitini na baada ya kujaribu kuzuwiwa na maafisa wa usalama mmoja alijiripua mbele ya waumi waliokuwepo karibu na mwengine akafanikiwa kuingia msikitini kupitia dirishani na kujilipua huko.

Hakuna kundi lolote hadi sasa lililokiri kuhusika na mashambulio yote mawili.