1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wawili wauawa huku maandamano yakiendelea Kashmir

21 Agosti 2019

 Watu wawili wameuawa katika shambulizi la ufyetulianaji risasi leo Jumatano(21.08.2019)katika eneo la Kashmiri linaloongozwa na India huku vikwazo vya mawasiliano na kutembea kulegezwa.

https://p.dw.com/p/3OHeg
Pakistan Kaschmir Protest & Unruhen in Lahore
Picha: Reuters/M. Raza

Msemaji wa polisi amesema kuwa mtu anayeshukiwa kuwa mwanamgambo na afisa mmoja wa polisi waliuawa katika mapigano hayo katika wilaya ya Baramulla. Afisa mwengine wa polisi alijeruhiwa wakati wanamgambo walipokuwa wakifyetua risasi wakati wa operesheni ya msako.

Haya ni mapigano ya kwanza yalioripotiwa kati ya waasi na vikosi vya maafisa wa usalama tangu serikali hiyo ya shirikisho kuondoa hadhi maalumu ya jimbo la Jammu na Kashmir na kuligawanya katika ngome mbili zinazosimamiwa na shirikisho hilo.

Eneo la Kashmir linaloongozwa na India lenye idadi kubwa ya waislamu limeshuhudia vuguvugu la ghasia la kutaka kujitenga tangu mwaka 1980 ambapo zaidi ya watu elfu 45 ikiwa ni pamoja na waasi, maafisa wa kikosi cha usalama na raia waliuawa.

Maelfu ya vikosi  zaidi vya kijeshi vilipelekwa katika bonde la Kashmir mkesha wa hatua ya serikali ya shirikisho kuondoa hadhi hiyo maalum. Hadhi hiyo ilitoa fursa kwa eneo hilo kujifanyia maamuzi katika maeneo mengi  ikiwa ni pamoja na kubuni sheria zake na kudhibiti ununuzi wa mali mbali na kutengeneza nafasi za kazi za serikali kwa watu wa eneo hilo.

Vikosi hivyo vilifuatilia mienendo ya watu katika mji mkuu wa eneo hilo Srinagar na miji mingine ya bonde la Kashmir kwa kutumia vizuizi vya barabarani na maeneo ya ukaguzi. Njia zote za mawasiliano ikiwa ni pamoja na simu za rununu na mtandao wa intaneti zimekatizwa tangu Agosti 4.

Kaschmir Protest & Unruhen in Srinagar
Waandamanaji warusha mawe dhidi ya wanajeshi mjini SrinagarPicha: picture-alliance/AP Photo/D. Yasin

Serikali yalegeza vikwazo 

Serikali ilianza kulegeza vikwazo hivyo wiki mbili baadaye huku afisi za serikali na shule za msingi katika mji huo wa Srinagar zikifunguliwa siku ya Jumatatu. Kulingana na msemaji wa serikali, siku ya Jumatano asilimia 90 ya wafanyikazi wa serikali walikuwa afisini huku mabasi maalumu yakiwabeba wafanyikazi kwenda kazini.

Hata hivyo shule nyingi hazikuwa na wanafunzi huku wazazi wakihofia kuwapeleka watoto wao shuleni kwa kukosa mawasiliano ya simu. Kulingana na mzazi mmoja, ameliambia shirika la habari la dpa kwamba dirisha la basi moja la shule lilivunjwa wakati mawe yaliporushwa katika eneo la Aluchibag kwa hivyo hakuna mzazi atakayethubutu kuwapeleka watoto wao shuleni.

Kulingana na walioshuhudia, kulikuwa na uvamizi kadhaa siku ya Jumanne usiku katika mji wa Telbal Kaskazini mwa Kashmir. Wameongeza kuwa vijana waliojiunga na maandamano mbali mbali na kurusha mawe dhidi ya vikosi vya kijeshi walikamatwa na vikosi vya usalama. Makundi madogo yaliandaa maandamano katika maeneo ya Fatehkadal na Soura miongoni mwa maeneo mengine.

Kulikuwa na msongamano mkubwa wa magari katika barabara nyingi lakini maduka mengi na biashara zilifungwa.Pakistan na India zote zinadhibiti sehemu ya Kashmir lakini kila moja inadai kumiliki eneo zima . Mataifa hayo jirani yamepigana vita viwili kuhusiana na eneo hilo.