1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wawili wajeruhiwa katika shambulizi la kisu Berlin

1 Januari 2025

Watu wawili walijeruhiwa katika shambulizi la kisu magharibi ya mji mkuu wa Ujerumani Berlin. Shambulizi hilo limeitikisa Ujerumani siku chache tu baada ya shambulizi kali la soko la Krismasi katika mji wa Magdeburg.

https://p.dw.com/p/4oiqF
Afisa wa polisi asimama nje ya duka la jumla ambako shambulizi la kisu liliwajeruhi watu wawili
Ujerumani ipo katika tahadhari kubwa baada ya shambulizi la soko la Krismasi kuwaua watu watano huko MagdeburgPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Msemaji wa polisi Bibi Jane Berndt amesema shambulio la jana la Mkesha wa Mwaka Mpya lilitokea katika wilaya ya magharibi ya Charlottenburg.

Polisi imesema maafisa wa huduma za dharura walifahamishwa kuhusu tukio hilo muda mfupi kabla ya saa sita mchana. Shambulizi hilo limeitikisa Ujerumani siku chache tu baada ya shambulizi kali la soko la Krismasi katika mji wa Magdeburg

Gazeti la Berliner Morgenpost liliripoti kuwa shambulio hilo lilianzia ndani ya duka la jumla. Polisi imesema mtu huyo aliyekuwa na kisu alitoka nje akitumia barabara ya wapitanjia karibu na hoteli moja iliyoko karibu.

Mshukiwa huyo, raia wa Syria anayeishi Sweden, inasemekana aliwavamia waathirika na kisu alichoiba kwenye duka la jumla. Watu wawili walilazwa hospitali na mshukiwa akakamatwa.

Katika tukio jingine tofauti la Mkesha wa Mwaka mpya, polisi ilimpiga risasi na kumuuwa mtu mmoja baada ya kuiba tingatinga ya kuchimba mchanga kusini magharibi mwa Ujerumani.

Maafisa watatu walimfuata mshukiwa huyo katika mji wa Grünsfeld baada ya kuendesha tingatinga hiyo mbele ya duka la vifaa.

Mshambuliaji huyo alitambuliwa kuwa Mjerumani mwenye umri wa miaka 38.