Watu 40 wauawa Israel katika mashambulizi ya Hamas
7 Oktoba 2023Takwimu hizo zimetolewa na kitengo cha Israel cha magari ya kuwabeba wagonjwa ikisema kuwa idadi hiyo inajumuisha watu waliouawa kwa maroketi na katika hujuma za ardhini.
Hamas imefyatua maroketi 2,200 kutokea Ukanda wa Gaza, katika kile ilichokitaja kuwa ni ''operesheni ya kijeshi.''
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema nchi yake iko vitani, na kuongeza kuwa maadui wa Israel ''watalipa gharama kubwa kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa''.
Soma pia:Baada ya shambulio la Hamas, Netanyahu asema Israel iko vitani
Pande mbali mbali duniani, zikiwemo Marekani, Umoja wa Ulaya na jumuiya ya kujihami ya NATO zimelaani mashambulizi hayo ya Hamas, na kuelezea mshikamano na Israel na watu wake.
Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas amesema Wapalestina wanayo haki na kujilinda, huku Saudi Arabia na Misri zikizitaka pande zote kuwa na ustahimilivu.
Wakati huohuo, wizara ya afya ya Gaza imesema kuwakaribu watu 200 wameuwawa baada ya mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la Israeli katika ukanda huo kama hatua ya kujibu mashambulizi. Watu wengine 1600, wamejeruhiwa katika tukio hilo.