Watu milioni moja hatarini Syria
22 Novemba 2016Takriban watu milioni moja wanaishi katika maeneo yanayoshambuliwa nchini Syria. Idadi hiyo ikiwa ni maradufu ya hali ilivyokuwa miezi sita iliyopita. Hayo yamesemwa na Umoja wa Mataifa.
Naibu Katibu anayesimamia Masuala ya kibinadamu ambaye pia ni mratibu wa misaada ya dharura katika Umoja wa Mataifa Stephen O' Brien ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa watu laki tisa, sabini na nne elfu na themanini wanazingirwa katika mazingira ya mashambulio.
Tangu mwezi Julai, watu laki mbili na elfu sabini na tano wamezidi kuwa hatarini, mashariki mwa Aleppo pekee, ambako vikosi vya serikali vimekuwa vikishambulia kuwalenga waasi. Steffan O'Brien anasema. "Hali ya kibinadamu mashariki mwa Aleppo imepita kuwa ya kutisha na sasa inatisha zaidi na sasa ni vigumu sana kustahimilika na binadamu".
Ameongeza kuwa raia wanatengwa, wanakabiliwa na njaa, wanashambuliwa kwa mabomu na kunyimwa huduma za kiafya na misaada ya kibinadamu ili kuwalazimisha kusalimu amri au waondoke. Ni mbinu makusudi ya kidhalimu kuwanyanyasa raia kuafikia malengo ya kisiasa, kijeshi na kwa namna nyingine kiuchumi. O' Brien anasema dhamira ya rais Bashar al-Assad ni kuharibu na kuangamiza raia wasioweza kujilinda wenyewe. Anees Rajab ni mkaazi wa Moadamiya Syria na anasema "Ninatumai tu kuwa wafungwa wataachiliwa haraka iwezekanavyo. wanangu wawili wa kiume na jamaa zangu wanne wangali katika jela. Hilo ndilo tumaini langu pekee".
Maeneo mapya ambayo yamekuwa katika hatari katika miezi ya hivi punde ni pamoja na Joubar karibu na Damascus, al-Hajar al-Aswad, Khan al-Shih na sehemu nyinginezo mashariki ya Ghutah na mashariki ya Damascus.
Utathmini wa O'Brien umejengwa kwenye wasiwasi wa jumuiya za kimataifa kuhusu hatima ya Aleppo hasa ikizingatiwa kuwa kuna watu laki mbili na nusu ndani yake mji huo unapoendelea kushambuliwa vikali kwa lengo la majeshi ya muungano wa Syria na Urusi kuukomboa kutoka mikononi mwa waasi.
Kundi la waangalizi la kutetea haki ya kibinadamu lenye makao yake Uingereza limesema zaidi ya watu 100 wameuawa mashariki mwa Aleppo katika kipindi cha wiki moja iliyopita.
Wakati uohuo, mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa nchini Syria Staffan de Mistura alifeli kuafikia mkataba na serikali ya Assad wa kuboresha hali ya kibinadamu.
Mwandishi: John Juma DPAE/AFPE
Mhariri: Yusuf Saumu