Watu mashuhuri 225 wataka mataifa tajiri kusaidia masikini
2 Juni 2020Na pia watu hao mashuhuri wametaka mataifa hayo tajiri kuanzisha ufufuaji wa uchumi kutokana na janga hilo, hususan kwa mataifa yanayoendelea yaliyoathirika zaidi na yale yenye uchumi wa kati.
Watu hao washuhuri wamesema katika barua kwamba mataifa haya masikini na yenye uchumi wa kati, ambayo yanawakilisha asilimia 70 ya idadi ya watu duniani na kwa wastani theluthi moja ya pato jumla la ndani la kila mwaka GDP, yanataka ichukuliwe hatua haraka. Zaidi ya mataifa 100 yameliendea shirika la fedha ulimwenguni IMF kutaka msaada, wamesema watu maarufu, na mengi zaidi yanatarajiwa kufanya hivyo.
Bila ya kuchukuliwa hatua kutoka kundi hilo la mataifa ya G20, watu hao mashuhuri duniani wameonya kuwa mdororo wa uchumi utakaosababishwa na janga la virusi vya corona utaongezeka, na kuathiri uchumi wa mataifa yote," na watu duniani ambao wametengwa na ni masikini wataathirika zaidi.
Msaada kwa mataifa masikini
Wamesema kuwa mataifa ya G20, kwa hivi sasa yakiongozwa na Saudi Arabia, yanawakilisha asilimia 85 ya pato jumla la ndani la wastani na yana, "uwezo wa kuongoza juhudi hizo za upatikanaji wa fedha katika kiwango kinachohitajika."
"Tuawataka viongozi kuchukua hatua mara moja," barua yao imesema. Waliotia saini ni pamoja na zaidi ya viiongozi wa zamani duniani 75, washindi watatu wa tuzo ya amani ya Nobel, washindi wanne wa nishani ya Nobel katika fani ya uchumi, katibu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, mfadhili George Soros, rais wa zamani wa benki kuu ya dunia James Wolfensohn, katibu mkuu wa zamani wa NATO Javier Solana pamoja na maafisa kadhaa wa zamani wa Umoja wa mataifa pamoja na wataalamu wa uchumi wa hivi sasa na wazamani,na wataalamu wa masuala ya kiutu na afya.
Mkutano wa kilele wa mataifa yenye uchumi mkubwa duniani ulianzishwa katika wakati wa mzozo wa kifedha mwaka 2008, lakini viongozi hao wamefanya mkutano mmoja kwa njia ya vidio tangu kuzuka kwa janga la ugonjwa wa COVID-19 duniani, na mkutano wao mwingine unapangwa kufanyika mwezi Novemba katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riayadh.
katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres amewahimiza viongozi wa kundi la mataifa ya G20 kabla ya mkutano huo mwishoni mwa mwezi Machi kuidhinisha mpango wa baada ya vita ikiwa ni pamoja na kichocheo cha uchumi, kwa kiwango cha trilioni za dola, kwa watu na biashara katika mataifa yanayoendelea kujaribu kupambana na janga la virusi vya corona.