1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 76 wafa na 1,000 hawajulikani walipo moto wa California

18 Novemba 2018

Idadi ya watu wasiojulikana walipo hadi sasa kutokana na moto mbaya kabisa jimbo la California, Marekani, imepindukia 1,200, huku mabaki ya miili 76 ikiwa imepatikana na msako ukiendelea.

https://p.dw.com/p/38Rii
USA Waldbrände in Kalifornien
Picha: Imago/Xinhua/Zhao Hanrong

Tathmini iliyotolewa na mkuu wa Kaunti ya Butte ulitokea moto huo, Kory Honea, alisema siku ya Jumamosi (Novemba 18) kwamba ongezeko la idadi ya watu wasiojulikana walipo linatokana na juhudi za ofisi yake kuchunguza idadi ya simu za dharura zilizopigwa wakati wa masaa ya awali ya moto huo kuanza mnamo tarehe 8 Novemba.

Timu za uchunguzi ziligundua mabaki ya watu watano zaidi siku ya Jumamosi, na kuifanya idadi ya waliothibitishwa kupoteza maisha hadi sasa kufikia 76, ambapo 63 tayari wameshatambuliwa katika ngazi za awali, wakingojea sasa vipimo vya vinasaba.

Kwa mujibu wa Honea, maafisa wa kaunti hiyo sasa wanapitia orodha ya watu wasiofahamika walipo kwa kulinganisha na wale waliofanikiwa kukimbia, ambapo watu 380 wametambulika walipo na kuondolewa kwenye orodha hiyo tangu Ijumaa.

"Kuna hatua kubwa zimepigwa kwenye hilo, lakinji bado takwimu hizi hazijachambuliwa," alisema mkuu huyo wa Kanuti ya Butte.

Trump atembelea eneo la maafa

USA Waldbrände in Kalifornien | Abgebranntes Haus
Mfanyakazi wa huduma za uokozi akikusanya mabaki kwa ajili ya uchunguzi kwenye eneo lililoteketezwa kwa moto Camp Fire, mji wa Paradise, jimbo la California.Picha: Reuters/T. Sylvester

Honea alizungumza baada ya Rais Donald Trump kutembelea mji mdogo wa Paradise ambao ulikuwa ukikaliwa na watu takribani 27,000 kwenye milima ya Sierra, umbali wa kilomita 280 kutoka mji mkuu wa California, San Fransisco. Mji huo sasa kwa ujumla umeteketezwa wote.

"Hakuna ambaye aliwazia jambo hili lingeliweza kutokea," Trump aliwaambia waandishi wa habari akiwa kwenye eneo la tukio. 

"Ni jambo la kusikitisha sana kulishuhudia. Hakuna anayejuwa watu wangapi wamepoteza maisha yao hapa. Kwa sasa tunataka tuwahudumie wale waliojeruhiwa vibaya," alisema Trump akiwa ameambatana na Gavana Jerry Brown wa California na gavana mteule, Gavin Newsom. 

Hata hivyo, alipoulizwa endapo moto huo umebadili mawazo yake kuhusu hatari za mabadiliko ya tabianchi, Trump alisema: "Hapana. Hoja yangu haijabadilika. Ninataka tabianchi iliyo imara na tutaipata na tutakuwa na misitu iliyo salama."

Brown alisema serikali ilikuwa ikifanya kile ilichopaswa kukifanya, ikiwemo kuwasaidia waokoaji, kusafisha eneo na kuwasaka wahanga wa maafa haya.

Tayari janga hili linatajwa kuwa miongoni mwa majanga mabaya kabisa kwa karne hii. Watu 87 waliangamia kwa moto kwenye eneo la Big Burn mnamo mwaka 1910, ambapo moto mwengine kwenye eneo la Minnesota uliuwa watu 450 mwaka 1918.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Yusra Buwayhid