1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 6 wauawa Lebanon

27 Desemba 2013

Watu sita, akiwemo waziri wa zamani wa fedha wa Lebanon, Mohamad Chatah, wameuawa katika mripuko wa bomu uliotokea Beirut. Mauaji hayo yalitokea wakati Chatah akielekea kwenye mkutano wa wanasiasa wa nchi hiyo, Beirut.

https://p.dw.com/p/1AhYz
Mji wa Beirut, baada ya kutokea mripuko
Mji wa Beirut, baada ya kutokea mripukoPicha: Reuters

Shirika la habari la taifa-NNA limeripoti kuwa Chatah ambaye ni mpinzani mkubwa wa Rais Bashar al-Assad wa Syria pamoja na mlinzi wake ni miongoni mwa watu waliouawa katika shambulio hilo la leo (27.12.2013) lililotokea kwenye eneo la bahari na kwamba gari walilokuwa wamepanda limeharibiwa kabisa.

Chatah aliyekuwa na umri wa miaka 62, aliwahi kuwa balozi wa Lebanon nchini Marekani na mshauri wa waziri mkuu wa zamani wa Lebanon, Fuad Siniora na pia aliendelea kubakia mshauri wa karibu wa mrithi wa Siniora, Saad Hariri.

Hariri aishutumu Hezbollah

Hariri amelishutumu kundi la Lebanon la wapiganaji wa Hezbollah la Waislamu wa madhehebu ya Shia kuhusika na mauaji hayo na kwamba huo ni ujumbe mpya kuhusu ugaidi.

Waziri mkuu wa zamani wa Lebanon, Saad Hariri
Waziri mkuu wa zamani wa Lebanon, Saad HaririPicha: AP

Hariri amesema kuwa watuhumiwa wa mauaji hayo ni wale wanaoikimbia sheria ya kimataifa na wanaokataa kujisalimisha kwenye mahakama ya uhalifu. Rais wa Lebanon, Michel Suleiman na Waziri Mkuu Najib Mikati, pamoja na maafisa wa makundi ya kidini na kisiasa, wamelaani mauaji hayo ya Chatah.

Mikati amesema bomu hilo lilimlenga mwanasiasa aliyekuwa anapenda na kuamini katika mazungumzo. Naye mbunge wa Hezbollah, Ali Ammar ameyaelezea mauaji hayo kama uhalifu na wanalaani kitendo hicho cha kigaidi.

Mauaji hayo yametokea wiki tatu kabla la kuanza kwa kesi ya wapiganaji watano wa Hezbollah wanaotuhumiwa kumuuwa waziri mkuu wa zamani, Rafik Hariri na watu wengine 21 mwaka 2005. Chatah aliyekuwa Muislamu wa madhehebu ya Sunni, alikuwa mkosoaji mkubwa wa Hezbollah.

Hezbollah haiwezi kutawala Lebanon

Waziri wa zamani wa Lebanon, Marwan Hamadeh, aliyesalimika shambulio la bomu la kutegwa kwenye gari mwaka 2004, amesema kundi la Hezbollah haliwezi kutawala nchini Lebanon, hata kama litavuruga amani na kusababisha umwagikaji mwingi wa damu.

Rais wa Syria, Bashar al-Assad
Rais wa Syria, Bashar al-AssadPicha: Reuters

Lebanon imekumbwa na mashambulizi kadhaa ya mauaji yanayohusishwa na vita vya Syria, yakiwemo mashambulizi mawili ya kujitoa mhanga kwenye ubalozi wa Iran mjini Beirut mwezi Novemba na kuwaua watu 25.

Mzozo wa Syria umedhoofisha usalama wa Lebanon na kuongeza mvutano wa kimadhehebu. Hezbollah imepeleka wapiganaji wake Syria kumuunga mkono Rais Assad, ambaye anatokea katika jamii ya Alawi ambayo ni sehemu ya Washia.

Baadhi ya makundi ya waasi ya Waislamu wa madhehebu ya Sunni nchini Syria yana mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda na yamekuwa yakijaribu kuung'oa madarakani utawala wa Rais Assad.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE,APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman