1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 6 wafariki katika siku ya uhuru Marekani

5 Julai 2022

Mauaji ya watu sita yaliyofanywa na mtu aliyejihami kwa bunduki huko Chicago, Marekani Jumatatu, yametilia kiwingu maadhimisho ya siku ya uhuru yanayofanyika kote nchini humo.

https://p.dw.com/p/4DedZ
Chicago: Schüsse bei Parade zum 4. Juli
Picha: Nam Y. Huh/AP/picture alliance

Haya yanafanyika katika wakati ambapo nchi hiyo tayari iko kwenye tafrani ya maamuuzi ya mahakama ya juu kuhusiana na uavyaji mimba na umiliki wa bunduki na pia jaribio la mapinduzi la Januari 6 katika majengo ya bunge.

Mauaji haya yamefanyika wakati ambapo nchi hiyo inajaribu kutafuta sababu ya kusherehekea kuanzishwa kwake na chanzo ambacho bado kinaishikilia nchi hiyo pamoja.

Ilistahili kuwa siku ambayo kila mmoja angechukua mapumziko kutoka kazini, ajiunge na magwaride na kufurahia mlo na familia na marafiki na kushuhudia fataki zikirushwa, ila sivyo ilivyokuwa, hasa katika mtaa wa kitajiri wa Highland Park, Chicago.

Biden kuendelea mapambano dhidi ya janga la bunduki

Gwaride la maadhimisho katika eneo hilo lilianza mwendo wa saa nne asubuhi ila dakika kumi baadae lilisitishwa baada ya milio ya risasi kusikika. Mamia ya waliohudhuria maadhimisho hayo, baadhi wakionekana wanavuja damu, walikimbia kutoka eneo hilo.

Chicago: Schüsse bei Parade zum 4. Juli
Baadhi ya vitu vilivyoachwa baada ya watu kukimbia kufuatia milio ya risasiPicha: WLS/ABC7/REUTERS

Mtu anayedaiwa kuhusika na ufyatuaji huo wa risasi Robert Crimo III mwenye umri wa miaka 22, alikamatwa na polisi baadae.

Katika hotuba yake ya siku ya uhuru, Rais Joe Biden amelaani mauaji hayo aliyoyataja kuwa ya "kikatili" na kuahidi kupigania kile alichokiita janga la machafuko yanayotokana na bunduki nchini Marekani.

"Kabla niondoke kwenda Ulaya, nilisaini sheria. Sheria ya kwanza ya kweli ya usalama wa bunduki katika kipindi cha miaka 30. Na mambo bado yatakuwa mazuri ila sio bila mapambano ya pamoja. Nyote mumesikia kilichotokea leo. Kila siku tunakumbushwa kwamba hakuna kilichodhaminiwa kuhusiana na demokrasia yetu. Hakuna kilichodhaminiwa kuhusiana na jinsi tunavyoishi. Ni sharti tukipiganie, tukilinde na kukipata kwa kupiga kura," alisema Biden.

Migawanyiko kufuatia uamuzi wa mahakama ya juu

Biden vile vile amesema yeye anaona Marekani iliyo na umoja zaidi kinyume na maoni ya wengi kwamba nchi hiyo imegawika.

US-Präsident Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Bastiaan Slabbers/NurPhoto/picture alliance

Kumekuwa na migawanyiko mikubwa ya kijamii na kisiasa kuhusiana na maamuzi ya hivi karibuni ya mahakama ya juu nchini Marekani, ya kuipindua haki ya kikatiba ya uavyaji mimba na kufutilia mbali sheria ya New York iliyokuwa inadhibiti mtu anayeweza kuruhusiwa kubeba bunduki hadharani.

Kwa wengi siku ya uhuru ya Julai 4 ilikuwa ni fursa ya kuziweka kando tofauti za kisiasa na kusherehekea umoja, kukumbuka mapinduzi yaliyozaa demokrasia iliyodumu kwa kipindi kirefu zaidi katika historia.

Chanzo:AFP/APE