Watu 200 wauawa eneo la Karamoja tangu mwaka huu uanze
7 Julai 2020Matangazo
Jeshi la Uganda UPDF limethibitisha kuuawa kwa watu 200 eneo la Karamoja katika kipindi cha miezi sita tangu mwanzoni wa mwaka huu. Mauaji hayo yamehusiana hasa na wizi wa mifugo ambao umeshamiri katika eneo hilo linalopakana na Kenya na Sudan Kusini.
Msemaji wa jeshi hilo eneo la Kaskazini Mashariki mwa Uganda Meja Peter Mugisa ameeleza kuwa Alhamisi wiki iliyopita, genge la wezi 500 waliojihami kwa bunduki na silaha zingine walivamia wilaya ya Kaabong na kuiba ng'ombe 800.
Wezi hao walijaribu kuwavusha wanyama hao kuwaingiza Kenya katika eneo la mpaka la Turkana.
Katika operesheni hizo za kupambana na wezi wa mifugo, ng'ombe 8,484 wamekombolewa kutoka kwa wezi hao. Bunduki 68 zimepatikana kutokana na juhudi hizo tangu mwanzo wa mwaka huu.