1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Watu 19 wameripotiwa kuuawa kwa shambulizi la Israel, Gaza

12 Oktoba 2024

Watu 19 wameripotiwa kuuawa katika eneo la Jabalia kaskazini mwa Gaza kufuatia mashambulizi ya anga na ardhini yaliyofanywa na jeshi la Israel usiku kucha.

https://p.dw.com/p/4lifx
Gaza
Wakazi wa Gaza wakiwa wanaondoka katika eneo la kaskazini mwa mji huo kufuatia kuongezeka kwa mashambulizi ya IsraelPicha: OMAR AL-QATTAA/AFP

Watu 19 wameripotiwa kuuawa katika eneo la Jabalia Kaskazini mwa Gaza kufuatia mashambulizi ya anga na ardhini yaliyofanywa na jeshi la Israel usiku kucha. Mashambulizi hayo yamefanyika wakati jeshi la Israel likiendelea kupenya ndani zaidi mwa eneo hilo. 

Jeshi hilo lilichapisha amri mpya kuwataka watu waondoke katika vitongoji viwili vya kaskazini mwa mji wa Gaza na kusema kuwa ni eneo hatari la mapigano. 

Wakati huohuo, jeshi la Israel limewaamuru wakaazi wa vijiji 23 vya kusini mwa Lebanon kuondoka katika maeneo yao na kuelekea upande wa kaskazini ya Mto Awali.

Soma zaidi. Lebanon yatoa wito wa kusitishwa vita vya Israel na Hezbollah

Maeneo hayo yanatajwa na jeshi la Israel kuwa ni ngome ya kundi la Hezbollah kuficha silaha zao na kuanzisha mashambulizi dhidi ya Israel.

Katika hatua nyingine kundi la Hezbollah limesema limelishambulia kwa droni eneo la kambi ya jeshi la anga kwenye mji wa Haifa, kaskazini mwa Israel. Mashambulizi hayo yamefanyika saa chache baada ya kundi hilo hilo kusema lilihusika na shambulio jingine katika kambi ya jeshi kusini mwa mji huo.