Watu 13 wauawa katika shambulizi la gari mjini Barcelona
18 Agosti 2017Polisi nchini humo wamethibitisha tukio hilo kuwa ni shambulizi lakigaidi. Dereva wa gari hilo ametoweka na bado anaendelea kusakwa. Tayari watu wawili wanaoshukiwa kuhusika na tukio hilo wametiwa mbaroni huku mtu mmoja akiuawa baada ya kuendesha gari kupita kizuizi cha polisi kwa ajili ya ukaguzi.
Afisa mmoja wa taasisi inayohusika na ulinzi wa raia nchini humo amesema miongoni mwa waliojeruhiwa katika tukio hilo ni raia wa mataifa ya kigeni kutoka Ufaransa, Ujerumani , Ubelgiji, Uholanzi, Australia, Argentina na Italia.
Bendera kupepea nusu mlingoti
Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy ametangaza siku tatu za maombolezo ambapo bendera nchini humo zitapepea nusu mlingoti.Wakati huohuo Kansela wa ujerumani Angela Merkel ametuma salaamu za rambirambi kwa serikali ya Uhispania kufuatia tukio hilo linalodaiwa kuwa ni shambulizi la kigaidi. Msemaji wa Kansela Merkel Steffen Seibert ameandika katika ukurasa wa twitter kuwa Kansela Merkel amesema anaungana na wananchi wa Uhispania katika kipindi hiki kigumu. Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May naye pia amelaani shambulizi hilo.
Mwandishi: Isaac Gamba/afpe
Mhariri :Iddi Sessanga