1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto milioni 303 hawaendi shule kote duniani

19 Septemba 2018

Watoto 303 milioni kote duniani hawaendi shule, huku zaidi ya theluthi moja ya idadi hiyo wakiwa wanaishi katika maeneo ya migogoro au nchi zinazokabiliwa na majanga ya asili.

https://p.dw.com/p/35BNS
UNICEF Schüler in Guinea-Bissau
Picha: UNICEF/UNI162094/Lynch

Mtoto mmoja kati ya watoto watatu na vijana walio na umri wa kati ya miaka mitano na kumi na saba wanaoishi katika mataifa yalioathirika na migogoro,104 milioni hawako shuleni. Idadi hiyo inachangia zaidi ya thuluthi mbili ya idadi ya watoto wote duniani wasiokwenda shule, kulingana na ripoti iliyotolewa na Hazina ya Umoja wa Mataifa inayowashughulikia watoto UNICEF.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa mtoto mmoja miongoni mwa watoto watano walio na umri wa kati ya miaka kumi na mitano na kumi na saba wanaoishi katika nchi zilizoathirika kwa majanga au vita hawajawahi kuingia katika shule, na wawili miongoni mwa watano hawajawahi kukamilisha elimu ya shule ya msingi.

Ripoti hiyo iliyoitwa´´Kizazi kijacho kilichoibiwa´´ imetathmini hali ya elimu ya watoto na vijana kutoka shule ya msingi hadi sekondari katika nchi mbalimbali zikiwemo zinazokabiliwa na dharura za kibinadamu. Mataifa kumi yaliyoathirika zaidi yote ni ya Afrika, na hali ni mbaya nchini Niger, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini na Eritrea.

Mkurugenzi wa UNICEF Henrietta Fore amesema kwamba watoto wanaoishi katika mataifa hayo yanayikabiliwa na migogoro ni waathiriwa wakuu.´´Katika muda wa hivi karibuni, shule zao zinaharibiwa, na kuchukuliwa na majeshi au hata kushambuliwa makusudi. Wao pamoja na mataifa wanayoishi yataendelea kukabiliwa na mizunguko ya umaskini.´´

UNICEF yapendekeza uwekezaji zaidi katika elimu

UNICEF Schulkinder in Mosambik
Picha: UNICEF/UNI46342/Pirozzi

Huku kukiwa na asilimia nne pekee ya ufadhili unaotolewa kwa masuala ya elimu kote duniani, ripoti hiyo inapendekeza kuwepo kwa uwekezaji zaidi. Uwekezaji huo unafaa kuwa katika elimu bora ambapo watoto na vijana wanaweza kusoma kwenye mazingira salama, kutoka shule za msingi na sekondari.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa kabla ya mkutano wa sabini na tatu wa Bunge la Umoja wa Mataifa unaotarajiwa kuandaliwa wiki ijayo, imetathmini hali duniani ya watoto ambao hawako shuleni, vilevile kwamba kote duniani nusu ya watoto ambao hawahudhurii masomo ya msingi wanaishi katika nchi zilizo na dharura.

Kadhalika imetaja kuwa umaskini ndio kizingiti kikubwa kwa upatikanaji wa elimu duniani, huku watoto wanaotoka familia zisizojiwezza wakiwa na uwezekano mara nne ya kukosa shule wakilinganishwa na wenzao wanaotoka katika familia za kitajiri.

Kulingana na mwenendo wa sasa, idadi ya vijana walio kati ya umri wa miaka kumi na kumi na tisa itaongezeka kwa zaidi ya bilioni 1.3 ifikapo mwaka 2030, ambalo ni ongezeko la asilimia nane.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/DPAE/UNICEF

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman