Watoto milioni 28 wang'olewa makwao na vita
7 Septemba 2016Ripoti iliyotolewa jana na shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia watoto la UNICEF limegundua kuwa huku watoto wakiwakilisha thuluthi moja ya idadi ya watu duniani, asilimia hamsini ya wakimbizi duniani pia ni watoto. Hiyo inamaanisha kuwa kwa kila watoto 200 duniani, mmoja ni mkimbizi.
Idadi ya watoto walio wakimbizi imeongezeka maradufu katika kipindi cha muongo mmoja uliopita. Mkurugenzi wa mipango wa UNICEF Ted Chaiban amesema watoto wanastahili kulindwa na kupewa huduma muhimu kama elimu.
Kulingana na ripoti ya UNICEF kuna takriban watoto milioni 10 wakimbizi na watoto milioni moja wanaotafuta hifadhi ambao bado hatma yao haijulikani. Watoto wengine milioni 17 ambao wamelazimika kuyahama makaazi yao kutokana na vita na mizozo wanasalia katika maeneo ya mipaka katika nchi zao.
Watoto wengi wakimbizi ni Wasyria na Wafghani
Umoja wa Mataifa umesema asilimia 45 ya watoto hao walioathirika na vita na mizozo wanatoka nchi mbili, Syria na Afghanistan. Wengi wa watoto hao wanaotoroka mizozo wanasafiri bila ya kuandamana na watu wazima.
Kiasi cha watoto laki moja waliwasilisha maombi ya kupewa hifadhi katika nchi 78 mwaka 2015 hiyo ikiwa ni mara tatu idadi ya walioomba hifadhi mwaka 2014. Wengi wao wanatumika vibaya na kuwa katika hatari kwasababu hawana vitambulisho wala hadhi kisheria ya kuwa raia au waomba hifadhi katika nchi wanazofikia, hakuna mfumo wa kufuatalia na kukidhi maslahi yao.
UNICEF inakadiria kuwa watoto wengine milioni 20 ni wahamiaji wanaolazimika kuhama makwao kutokana na umasikini, ghasia, mashambulizi kutoka kwa magenge, miongoni mwa mazingira mengine yanayohatarisha maisha yao.
UNICEF: Jumuiya ya kimataifa iwaokoe watoto
Watoto hao wanakabiliwa na hatari ya kuzama baharini wakati wanaposafiri, utapia mlo, kukosa maji mwilini, kutekwa nyara, ubakaji na mauaji na wanapowasili katika nchi nyingine wanakumbwa na ubaguzi na chuki dhidi ya wageni.
Ripoti hiyo ya UNICEF iliyopewa jina 'Kung'olewa' inaitaka jumuiya ya kimataifa kuwalinda watoto, kuwapa elimu, huduma za afya na kuzitaka serikali kushughulikia chimbuko la linalochochea watu kuzihama nchi zao na kuwa wakimbizi na wahamiaji.
Ripoti hiyo imetolewa kabla ya mikutano miwili ya kilele itakayojadili mzozo wa wakimbizi duniani itakayofanyika tarehe 19 na 20 mwezi huu, pembezoni mwa mkutano mkuu nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Mmoja wa mikutano hiyo utaongozwa na Rais wa Marekani Barack Obama.
Viongozi wa dunia wametakiwa kuongeza juhudi za kuhakikisha familia zinaishi pamoja na kujizuia kuwashikilia watu vizuizini ili kupunguza idadi ya watoto wanaojikuta pekee yao katika mazingira hatari wanapovitoroka vita.
Mwandishi: Caro Robi/ap/Reuters/afp
Mhariri: Saumu Yusuf