Watetezi wa mazingira zaidi ya 200 waliuawa mwaka 2017
24 Julai 2018Shirika la kimataifa la Global Witness limesema kwamba limerikodi visa 207 vya wanaharakati waliouawa wakati wakijaribu kuilinda ardhi dhidi ya shughuli za kibiashara, mara nyingi kwa ajili ya ulimaji wa kahawa na michikichi, na kuufanya mwaka 2017 kuwa mwaka mbaya zaidi katika rikodi ya mauaji ya wanaharakati wa mazingira.
"Wakati mahitaji ya bidhaa hizi dunaini yakiongezeka, kuna kinyang'anyiro miongoni mwa wafanyabiashara kujipatia kiasi kikubwa cha ardhi wanachohitaji ili kupanda mazao hayo", alisema Ben Leather, mtetezi mwandamizi kutoka Global Witness. Leather anasema "pale watu wanaposimama kudai haki zao na kutaka mazingira yao yalindwe, wananyamazishwa kikatili".
Shirika hilo limesema limepata ushahidi kwamba maafisa wa serikali kama vile wanajeshi au polisi wanahusika angalau na vifo 53. Mtetezi huyo anasema katika kesi nyingi, maafisa wa serikali waliwaua watu kwa bunduki lakini katika visa vyengine serikali iliwaruhusu wafanyabiashara kuingia bila ya kulinda haki za wananchi wanaomiliki ardhi, na kwa hiyo wanashiriki kwenye mauaji ya wanaharakati.
Ripoti ya Global Witness juu ya mauaji ya wanaharakati wa mazingira inabainisha uhalifu duniani kote dhidi ya jamii zinazodiriki kupaza sauti dhidi ya wafanyabiashara wakubwa na serikali. Uhalifu huo unajumuisha mauaji, lakini vitisho, kukamatwa, mashambulizi ya mtandaoni, unyanyasaji wa kingono na mashitaka.
Kilimo cha biashara, uchimbaji madini, ukataji miti na ujangili ni shughuli zinazozalisha bidhaa za kila siku kama vile mafuta ya mchikichi kwa ajili ya vipodozi, soya kwa ajili ya nyama na mbao kwa ajili ya samani.
Brazili ndiyo imekuwa nchi hatari mwaka 2017 dhidi ya watetezi wa ardhi ikiwa na vifo vya watu 57, Ufilipino inafuatia ikiwa na vifo vya watu 48. Leather anaendelea kusema kwamba "serikali ina jukumu la kisheria na kimaadili kuwalinda watetezi wa haki za binadamu lakini kikawaida wanawashambulia kama takwimu zinavyoonesha, kupitia vikosi vyenye silaha vinavyofanya mauaji hayo".
Mbali ya kuwa mwaka mbaya kwa watetezi wa mazingira tangu shirika la Global Witness lilipoanza kuorodhesha vifo vyao, mwaka 2017 ulishuhudia pia mauaji zaidi ya wanaharakati wa ardhi katika historia. Shirika hilo lilibaini visa saba ambapo zaidi ya wanaharakati wanne waliuawa wakati mmoja, ikiwemo mauaji ya wanakijiji wanane waliokuwa wakipinga kilimo cha kahawa nchini Ufilipino.
Waathirika wakubwa wamekuwa ni wenyeji wa asili wa maeneo hayo, ambao mara nyingi tayari wametengwa na serikali pamoja na jamii. Pamoja na kutoa wito wa uwajibikaji na ulinzi zaidi wa jamii zilizo katika hatari kubwa, Leather anasema wafanyabiashara wakubwa na hata walaji wanaweza kusaidia kupunguza vurugu kwa kutaka uwazi zaidi.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/afp
Mhariri: Mohammed Khelef