Watawala, usalama wakamatwa kwa rushwa, Burundi
27 Julai 2020Waziri wa mambo ya ndani anaye husika pia na usalama aliahidi kusimama kidete katika kubiliana na ulaji rushwa nchini humo.
Kwa mujibu wa msemaji kwenye wizara ya mambo ya ndani na usalama, askari polisi wengi tayari wamefutwa kazi na kutiwa jela baada ya kufumwa wakijihusisha na maovu mbali mbali likiwemo kosa la ulaji rushwa.
Pierre Nkurukiye msemaji kwenye wizara hiyo amesema tume iliyoundwa na wizara hiyo iliwafumania jijini hapa Bujumbura watu 16 miongoni mwao askari polisi 13 wakiwaomba raia rushwa na pesa walizokuwa wamepata pia zilioneshwa kwa vyombo vya habari.
"Kundi la watu 16, miongoni mwao polisi 13 na wengine wakiwa ni raia wa kawaida lilifumaniwa likijihusisha na makosa mbali mbali. Miongoni mwao askari polisi 5 walikutwa wakiomba rushwa kwenye kituo cha polisi. Askari mwingine mmoja alimuomba raia rushwa ya faranga elfu 20. Wengine askari wa 3 wakiwa pamoja na raia mmoja aliyekuwa dereva, walitumia gari la polisi wakiwa na silaha na kudai kuwa ni kamishna wa polisi. Hivyo waliwakamata watu wenye baiskeli na kuwatoza faini. Wote hao walifumaniwa jijini hapa Bujumbura.", alisema
Pia Mkoani Makamba kusini mwa nchi kuna kundi la watu 13 miongoni mwao askari polisi 4 waliokamatwa kwa tuhuma za kuwaibia raia wanaoingia nchini wakitokea Tanzania. Watu hao wamekuwa wakihojiwa na polisi ili wahusika wote katika mtandao huo waweze kutiwa nguvuni.
Mkoani Muramvya katikati mwa nchi watawala kadhaa wanasakwa kwa udi na uvumba wakituhumiwa kuhusika katika kuteketeza miti ya msitu wa taifa. Mkoani Bubanza mkuu wa kijiji cha Rungunga alikamatwa na kutiwa jela kwa tuhuma za kuwapiga raia na kuwaacha katimauti uti.
Pierre Nkurikiye amesema lipo pia kundi la askari polisi zaidi ya 10 wanao fungiwa mkoani Bubanza kwa tuhuma za kutumia gari za serikali muda usokuwa wa kazi na kuziibia vipuri.
Waziri wa mambo ya ndani na usalama Gervais Ndirakobuca katika mkutano wake wa kwanza na maafisa wakuu kwenye wizara hiyo aliahidi kulivalia juga swala la rushwa. Alisema "anayejuwa kuwa hawezi kushuhulikia faili yoyote pasina kufumbatishwa rushwa basi hana nafasi. Atakayefumwa hata awe kapokea franga elf 2 basi nitamsindikiza hadi kwenye mlango wa jela, utaratibu wa kutoka ataujua mwenyewe".
Baadhi ya raia wamekaribisha nguvu hiyo serikalini huku wakikosoa kuona walokamatwa hadi sasa ni polisi wadogo wado na raia wa kawaida huku vigogo wakisalia bila kukerwa.
Soma Zaidi:Rais Ndayishimiye ana jukumu la kuleta mageuzi Burundi
Amida ISSA, DW, BUJUMBURA