1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watawa 13 waachiwa huru Syria

Mjahida10 Machi 2014

Watawa waliotekwa nyara katika kijiji kimoja nchini Syria wameachiwa huru leo asubuhi kutokana na mpango usio wa kawaida, wa ubadilishanaji wafungwa katika takriban miaka mitatu ya mapigano nchini humo.

https://p.dw.com/p/1BMqg
Baadhi ya watawa walioachiwa huru
Baadhi ya watawa walioachiwa huruPicha: AFP/Getty Images

Hatua hii imetokea wakati shirika la haki za binaadamu la kimataifa- Amnesty International likitoa ripoti yake juu ya ukatili unaofanywa na jeshi la nchi hiyo katika vita hivyo vilivyosababisha mauaji ya maelfu ya watu.

Wapiganaji wa kundi la jihadi waliwateka nyara watawa hao 13 pamoja na wafanyakazi watatu wa nyumbani mnamo Desemba 3 katika kijiji cha kikristo cha Maalula, ambapo wakaazi wa mji huo bado wanazungumza lugha asilia ya Aramaic iliokuwa ikizungumzwa wakati wa Yesu Kristo, na kuwachukua katika mji uliokuwa karibu wa Yabrud.

Wanawake hao waliowasili usiku wa kuamkia leo katika kijiji kinachodhibitiwa na serikali cha Jdeidet Yabus karibu na mpaka wa Lebanon, waliripotiwa kujawa na uchovu huku wakiwashukuru wale waliofanya mazungumzo juu ya kuachiwa kwao.

Mmoja wa watawa akizungumza na vyombo vya habari baada ya kuachiwa huru
Mmoja wa watawa akizungumza na vyombo vya habari baada ya kuachiwa huruPicha: Reuters

"Tunataka kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyefanikisha sisi kuwepo hapa leo, twatoa shukrani pia kwa rais wa Syria Bashar Al Assad kwa kuwasiliana na mfalme wa Qatar Tamim Bin Hamad al-Thani” Alisema mmoja wa watawa wakati alipokuwa akizungumza na waandishi habari.

Mtawa huyo aliyekuwa amevalia nguo nyeusi aemsema, wapiganaji wa kiislamu wanaofungamanishwa na kundi la kigaidi la Al Qaeda, Al-Nusra Front, waliowateka nyara, waliwaweka katika hali nzuri wakati walipokuwa mikononi mwao na walipewa kila walichokihitaji.

Aidha kuachiwa kwa watawa hao kumekuja wakati kukiwa na mapigano makali karibu na eneo la Yabrud ikiwa ni kampeni ya jeshi la Syria linaloungwa mkono na vuguvugu lililo na nguvu la Hezbollah nchini Lebabon, kuangamiza maeneo ya waasi.

Human Rights Watch lazungumzia hatua iliochukuliwa

Kwa upande mwengine Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch nchini Uingereza Rami Abdel Rahman, amesema wafungwa wanawake 150 waliokuwa katika jela nchini Syria wameachiwa huru na wapo katika mabasi manne karibu na mpaka wa Syria na Lebanon.

Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binaadamu Human Rights Watch,Kenneth Roth
Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binaadamu Human Rights Watch,Kenneth RothPicha: picture-alliance/dpa

Rami amesema wanawake hao wameachiwa huru kufuatia mpango wa wabadilishanaji wafungwa uliowajumuisha watawa hao 13.

Rami Abdel Rahman amesema bado maelfu ya watu wakiwemo watoto wamefungiwa katika jela nchini Syria ambapo mateso makubwa ndio mfumo unaotumika ndani ya jela hizo.

Shirika la Amnesty International limetoa ripoti yake inayosema kuwa jeshi la Syria limekuwa likitumia mpango wa kuwanyima chakula kama mbinu moja ya kivita katika kambi ya wakimbizi nje ya mji mkuu wa Damascus.

Shirika hilo limesema watu takriban 200 wamefariki tangu jeshi lilipozingira kambi ya Yarmuk mnamo Julai mwaka wa 2013, ambapo msaada wa chakula na madawa ulikatizwa.

Wanajeshi waliotiifu kwa Rais Bashar Al Assad
Wanajeshi waliotiifu kwa Rais Bashar Al AssadPicha: Reuters

Mwezi huu wa machi utafikisha miaka mitatu ya ghasia za Syria tangu zilipoanza tarehe 15 mwezi machi baada ya kufanyika maandamano makubwa dhidi ya rais Bashar Al Assad maandamano yaliogeuka mapigano ya wenyewe kwa wenyewwe.

Mapigano hayo yamesababisha zaidi ya watu 140,000 kuuwawa huku raia wengine takriban milioni 2.5 wakikimbilia nchi jirani kwa usalama wao na wenghine milioni 6.5 wakiwa wakimbizi wa ndani nchini Syria.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman