1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watanzania wenye ulemavu wataka kanuni za wazi kuwahusu

Shisia Wasilwa
12 Agosti 2024

Watu wenye ulemavu wamewaomba wahudumu wa afya kujifunza haki za watu wenye walemavu hasa wanawake wajawazito wanaokwenda kujifungua au kupata huduma za afya.

https://p.dw.com/p/4jOFc
Changamoto za watu wenye ulemavu
Walemavu Tanzania waiomba serikali kubainisha kanuni zinazosaidia kuondoa ubaguzi dhidi yao katika uchaguzi Picha: Zulkarnain/XinhuaIMAGO

Watu wanaoishi na ulemavu nchini Tanzania wanaonyesha wasiwasi kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa na hivyo kuiomba serikali kuweka wazi kanuni zinazosaidia kuondoa ubaguzi kwa watu wa kundi hilo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu. 

Soma pia: Madhila ya mauaji ya walemavu wa ngozi

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam, katika mkutano wa  watu wenye ulemavu uliofanyika jijini hapa  na kuwakutanisha watu wenye ulemavu, wakiwamo viongozi wa serikali wenye ulemavu, asasi za kiraia na wadau wa serikali.

 Wakizungumza katika mkutano huo, uliondaliwa na taasisi ya watu wenye ulemavu, ya  Ikupa Trust kwa kushirikiana na asasi ya kiraia ya Foundation for Civil Society, watu wenye ulemavu wameibua changamoto zao hasa zinazowakumba wajawazito wenye ulemavu, wanapokwenda kupata huduma za afya, ikiwamo kujifungua.

 Akizungumza katika mkutano huo, Jonas Lubago, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) amesema moja ya changamoto kwa wajawazito wenye ulemavu, ni wahudumu wa afya na miundombinu ya huduma za afya.

Binti Jasiri Magreth: Mwenye changamoto ya kusikia

Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa watu wenye ulemavu wanataka serikali iweke wazi, kanuni zinazowaongoza kuhusu watu wenye walemavu, kuondoa ubaguzi kwa watu wa kundi hilo na kuzingatia wagombea wenye ulemavu. Lubago ameitaka serikali kuweka mazingira rafiki, ikiwamo miundombinu, vifaa, na  kuhimiza sifa za wagombea ziwe zenye ujumuishi.

Soma pia: Mapambano ya mwandishi albino dhidi ya unyanyapaa

Takwimu mpya za mwaka 2024, zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS), zimebaini kuwa Tanzania ina watu wenye ulemavu asilimia 11.4 ya watanzania wote. Kati yao, idadi kubwa ni wenye ulemavu wa macho ambao ni asilimia 3.6.

Mwanafunzi wa Shule ya Habari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaa, Rukaiya Abdallah, ambaye ni mlemavu wa macho amezungumzia hali jumla ya changamoto kwa watu wenye ulemavu:

Mshauri wa kitaalamu wa watu wenye ulemavu, Peter Mwita, amesema ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika masuala ya maendeleo ni mdogo na kwa mujibu wa utafiti wa sensa ya watu na makazi, watu wenye ulemavu hawashirikishwi kupitia mabaraza yao katika serikali za mitaa.

Mkutano huu ulijumuisha watu 600 wenye ulemavu wakiwamo madiwani na viongozi wa serikali za mitaa, ukilenga kuwajengea uelewa watu wa kundi hilo katika masuala ya sensa, Uchumi na fursa.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani,(WHO) ulimwenguni kote kunakadiriwa kuwa na watu wenye ulemavu bilioni 1.3 sawa na asilimia 16 ya idadi ya watu wote ulimwenguni, huku Tanzania ikiwa na watu wa kundi hilo wanaokadiriwa kuwa milioni tano, laki tatu na  arobaini na saba elfu, sawa na asilimia 11.4.