1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watalii 13,000 wakwamishwa na theluji kubwa Uswisi

9 Januari 2018

Theluji kubwa imeanguka na kuwakwamisha watalii karibu 13,000 katika kituo cha michezo ya kuteleza kwenye barafu cha Zermatt, katika jimbo la Valaisi nchini Sweden, huku umeme pia ukikatika jimboni humo.

https://p.dw.com/p/2qZpk
Schweiz Matterhorn Alpinismus Breithorn mit Matterhorn im Hintergrund
Picha: picture alliance/Robert Harding World Imagery

Theluji hiyo imezuwia barabara zote na treni zinazoelekea katika kijiji hicho cha mapumziko kilichoko katika jimbo la kusini mwa Uswisi la Valais, ambalo pia limekumbwa na kukatika kwa umeme, mkuu wa kituo hicho Janine Imesch ameliambia shirika la habari la AFP.

Kwa sasa "kuna watalii karibu 13,000 mjini Zermatt," alisema Imesch, huku tovuti ya treni ikionya kuwa kwa wakati huu hakuna uwezekano wa kuwasili wala kuondoka katika eneo hilo.

Barabara kuu imefunga tangu mapema Jumatatu, wakati huduma za treni zilisitishwa jioni, alisema. Mji wa Zermatt ni nyumbani kwa wakaazi karibu 5,500 na una uwezo wa kuhudumia watalii 13,400 katika hoteli za nyumba za kukodi zilizoko katika mji huo.

Lakini watalii waliokwama hawataweza kutumia fursa ya theluji iliopo kwa wingi kwa wakati huu, kutokana na hatari kubwa ya kutokea maporomoko ya theluji katika eneo hilo. "Haiwezekani kuteleza kwenye barafu au kukimbia, lakini hilo ni sawa. Ni mandhari ya kuvutia," alisema Imesch, na kuongeza kuwa "hakuna haja ya kutaharuki."

Schweiz Matterhorn Alpinismus Zermatt
Vijiji kadhaa katika jimbo la Valais havina umeme kufuatia hali mbaya ya hewa.Picha: picture alliance/chromorange/S. Vogel

Ndege ya uchunguzi inapangwa kutumw akatika eneo hilo kutathmini hali na namna ya kuendelea. Vijiji kadhaa vingine vya wilaya ya Valais, vilitengwa pia na kuanguka kwa theluji kubwa. Eneo la Simplon katika jimbo la Valai limepigwa na theluji yenye ukubwa wa mita 3.5 katika kipindi cha saa 24, limeripoti shirika la habari la ATS.

Maporomoko ya matope na mawe, na pia mafuriko, vimelaazimisha kufungwa kwa barabara kadhaa jimboni Valais, kama ilivyo hatari ya maporomoko ya theluji, ambayo polisi ya jimbo hilo imesema iko katika kiwango cha juu kabisaa cha kuweza kutokea.

Wakati huo huo mvua kubwa zimelaazimu watu karibu 20 kuondolewa katika kijiji kidogo cha Eyholz, na kitongoji cha Mottec kiliondolewa watu kama tahadhari, limeripoti shirika la utangazaji la RTS.

Mbali na Valais, mazoezi ya kwanza ya maandalizi ya kombe la dunia la kuteremka mlima katika mji wa Wengen, katika jimbo la Bern, yalifutwa siku ya Jumanne, kutokana na theluji kubwa na upepo mkali, wamesema waandamaji.

Upepo uliovuma usiku mzima kwa kasi ya hadi kilomita 200 kwa saa ulimaanisha pia kuwa kulikuwepo na uharibifu mkubwa wa miundombinu kwenye viwanja vya michezo, hasa eneo la kumalizia ambako mahema na majukwaa yalipigwa.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Saumu Yusuf