1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataalamu wataka gharama za huduma za intaneti kupunguzwa

15 Februari 2024

Wadau wa sekta ya teknolojia wamesema kuna haja ya kupunguza gharama za intaneti, bei za vifaa vya teknolojia na kuhakikisha matumizi jumuishi ya intaneti kwa makundi yote, pamoja na sera rafiki za matumizi ya digitali.

https://p.dw.com/p/4cRPQ
Afrika | Future Ready Summit in Dar es Salaam
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa akiwa na Waziri wa Habari na Mawasiliano, Nape Nnauye, aktika mkutano wa kile wa masuala ya teknolojia jijini Dar es Salaam, Februari 15,2024. Picha: Florence Majani

Mkutano Mkuu wa Kimataifa unaowakutanisha washirika wa kimkakati wa teknolojia, maarufu kama "Future Ready Summit," umefanyika Alhamisi jijini Dar es Salaam huku wadau wa sekta hiyo wakitilia mkazo masuala manne - kupunguzwa gharama za intaneti, kupunguzwa bei za vifaa vya teknolojia, matumizi jumuishi ya intaneti kwa makundi yote, wakiwamo wanawake, sera na sheria  rafiki za matumizi ya dijitali.

Wadau katika mkutano huo walielezwa kuwa ipo haja ya kuimarisha  miundombinu ya intaneti Tanzania,  kwani takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watu bilioni 2 duniani waishio vijijini bado wanakabiliwa changamoto ya upatikanaji wa intaneti.

Soma pia:Miaka 20 ya Smartphone Barani Afrika 

Washiriki katika mkutano huo uliondaliwa na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom, wametakiwa kuweka mikakati ya pamoja ili kuimarisha miundombinu ya teknolojia ya habari na mawasiliano, ujumuishi wa dijitali na fedha na kuwahamasisha watu kuchangamkia fursa za kidijitali.

Tansania Dar es Salaam | Waziri Mkuu Kassim Majaliwa| Future Ready Summit
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akihutubia katika mkutano wa kimataifa wa masuala ya Teknolojia. Leo Februari 15, 2024. Jijini Dar es Salaam, Tanzania. Picha: Florence Majani/DW

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kassim amewataka wadau kufanya tathmini ni kwa namna gani wanawake watashiriki katika uchumi wa kidiitali.

"Makampuni ya simu, wekeni gharama nafuu za intaneti ili kuhimiza wananwake kushiriki katika uchumi wa kidjitali. Tunatamani kuona kila mtanzania anapata intaneti mpaka vijijini," alisema Majaliwa, akiwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo w akila mwaka.

Waziri Mkuu Majaliwa aliitaka wizara husika ibebe changamoto za kisera na sheria zilizoainishwa na wadau ili kutengeneza mazingira rafiki ya matumizi ya kidijitali.

Tofauti ya matumizi kati ya wanaume na wanawake

Mkuu wa kitengo cha Mamlaka ya Masoko na Mazingira wa Umoja wa Mawasiliano (ITU), Sofie Maddens, pia alisisitiza suala la ushiriki wa wanawake katika matumizi ya dijitali.

Maddens alisema bado kuna ombwe kati ya wanawake na wanaume kwenye matumizi ya intaneti na vifaa vya teknolojia kwani asilimia 70 ya wanaume duniani wanatumia intaneti huku asilimia 65 tu ya wanawake ndio wanaotumia intaneti.

Vijana wa Kitanzania wapambana kuunda Satelaiti

"Ikiwa wanawake watakosa mtandao, ikiwa hawawezi kumudu gharama za kununua vifaa, au kujisikia salama wanapokuwa mtandaoni, tunawezaje kuwatarajia kufanya uvumbuzi ujao wa kuibadili dunia, au kushiriki katika uvumbuzi wa kidigitali."

Soma pia: TEKNOHAMA kuinua kilimo Afrika

Maddens amesisitiza kuwa ujio wa akili ya kubuni (AI) ni sehemu ya Maendeleo yaTeknolojia na tunatakiwa kushirikiana kuifahamu.

Mkurugenzi wa Vodacom, Phillipi Bassiimire alizungumzia nia ya kampuni hiyo kushusha gharama za vifaa vya digitali ili kupambana na mgawanyo wa kidigitali. Amehimiza ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kupambana na suala hilo.

Mkutano huu umewakutanisha wadau wa teknolojia na washirika wa kimkakati ili kujadili kwa pamoja masuala yanayochochea maendeleo ya teknolojia Afrika.