1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waswisi wapiga kura kudhibiti idadi ya wahamiaji

10 Februari 2014

Raia wa Uswisi wamepiga kura kuunga mkono pendekezo la kudhibiti idadi ya wahamiaji wanaoingia nchini mwao hatua ambayo serikali ya Uswisi imesema ni pigo kwani itaathiri uchumi wa nchi hiyo na uhusiano na Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/1B5xu
Picha: picture-alliance/dpa

Asilimia 50.3 ya wapiga kura nchini Uswisi wameunga mkono kudhibitiwa kwa idadi ya wahamiaji wa matabaka yote wanaoingia nchini humo. Pendekezo hilo hasa liliungwa mkono zaidi katika maeneo ya vijijini ilhali wapiga kura kutoka miji mikubwa kama Basel, Geneva na Zurich waliipinga kura hiyo ya maoni.

Hatua hiyo ya kuweka kiwango cha wageni wanaoingia inafuatia kampeini kabambe za dakika za mwisho mwisho kutoka kwa makundi ya kizalendo nchini humo yaliyozua hofu kuwa kuingia kiholela kwa wahamiaji kutasababisha ongezeko kubwa sana la watu nchini humo na kuongeza idadi ya waislamu.

Kura itakuwa na athari kubwa

Waziri wa sheria wa Uswisi, Simonetta Sommaruga, baada ya kura hiyo amesema hatua hiyo itakuwa na athari kubwa na za muda mrefu kwa nchi hiyo na hususan uhusiano wao na Umoja wa Ulaya kwani ni kuondoka kwa mfumo ulioko sasa wa kuwa na uhuru wa watu kuingia na kutoka.

Raia wa Uswisi wakipanga foleni kupiga kura kudhibiti wahamiaji
Raia wa Uswisi wakipanga foleni kupiga kura kudhibiti wahamiajiPicha: picture-alliance/dpa

Licha ya kuwa Uswisi sio mwanachama wa Umoja wa Ulaya, ina uhusiano wa karibu na umoja huo ulio na nchi wanachama 28. Nchi hiyo ilikuwa imekubaliana na umoja huo kuhusu masuala kadha wa kadha ya kushirikiana ikiwemo makubaliano ya kuruhusu raia wa umoja huo kuishi na kufanya kazi Uswisi bila ya masharti mengi ya uhamiaji na badala yake Waswisi pia wanaweza kufanya hivyo katika nchi wanachama wa Umoja huo.

Chini ya sheria za Uswisi, serikali sasa italazimika kuifanyia marekebisho mikataba yake kuhusu uhuru wa watu kuingia nchini humo ila bado haijabainika wazi kufikia sasa ni masharti gani yatawekwa ili kulifikia hilo na itakuwa lini sheria hizo za kudhibiti wahamiaji zitaanza kutekelezwa.

Tayari Uswisi ilikuwa imeziwekea nchi nane za Ulaya mashariki na Ulaya ya kati masharti ya kuruhusu wahamiaji kutoka nchi hizo miaka miwili iliyopita.

Hatua itawaathiri maelfu ya raia wa umoja wa Ulaya

Hatua hiyo iliyopitishwa na raia wa Uswisi inatarajiwa kuwa na athari kubwa kwani maelfu ya raia wa kigeni walio na kisomo kizuri hasa kutoka nchi za Ujerumani, Ufaransa, Italia na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya wako nchini humo.

Waziri wa Sheria wa Uswisi Simonetta Sommaruga
Waziri wa Sheria wa Uswisi Simonetta SommarugaPicha: Reuters

Kabla ya kura hiyo ya maoni ya hapo jana, makundi ya wafanyibiashara yalionya kuwa wengi wa watu 80,000 walioingia Uswisi mwaka jana ni muhimu kwa uchumi wa nchi hiyo na kuanzisha sheria za kudhibiti uhamiaji huenda zikasababisha hata Waswisi wenyewe kupoteza ajira.

Chama cha mabenki ya Uswisi kimeelezea kuvunjwa kwake moyo na kura hiyo na kusema kinahitaji kufanya mazungumzo muhimu na Umoja wa Ulaya kuelezea msimamo wao.

Umoja wa Ulaya umesema umesikitishwa na matokeo ya kura hiyo lakini utasubiri kuona jinsi serikali itakavyolishughulikia suala hilo baada ya wapiga kura kutaka sheria za uhamiaji zibadilishwe.

Vipengee vya kura hiyo ya maoni vinaipa serikali mamlaka ya kuamua ni wahamiaji wangapi wanaweza kuruhusiwa kuingia nchini humo kwa mwaka na pia inaitaka serikali kuanzisha kanuni za kupunguza haki za wahamiaji hao kuleta familia zao kupata huduma za kijamii na kukomesha maombi ya uhamiaji hatua ambayo huenda ikaimulika Uswisi kuhusu msimamo wake wa haki za binaadamu.

Mwandishi:Caro Robi/Ap/dpa

Mhariri: Josephat Charo