Washambuliaji wauwa 10, wajeruhi 15 kwa visu Canada
5 Septemba 2022Kamishna msaidizi wa polisi wa Canada, Rhonda Blackmore, aliwaambia waandishi wa habari kwamba jeshi lake lilipokea simu kutoka eneo linalokaliwa na jamii za wenyeji karibu na mji wa Weldon jimbo la Saskatchewan siku ya Jumapili (4 Septemba), ikisema kwamba watu 10 walikuwa wameuawa.
Kamishna huyo alithibitisha pia kuwa watu wengine 15 waliojeruhiwa walikuwa wamepelekwa katika hospitali mbalimbali za eneo hilo.
"Tuna maeneo 13 ya uhalifu tunayoyachunguza. Kwa hivyo, katika baadhi ya maeneo hayo kunaweza kukawa hakuna mtu aliyeuawa. Kunaweza kukawa na majeruhi ambao hawakuuawa. Kwa sasa msisitizo wetu ni kuwakamata washukiwa na kuwaweka ndani ili kuhakikisha usalama wa umma." Alisema kamishna huyo msaidizi wa polisi, akiongeza kuwa baadhi ya wahanga wa mauaji haya ya kushitukiza walilengwa na washambuliaji lakini wengine walishambuliwa ovyo ovyo.
Hata hivyo, polisi hadi sasa haijajuwa dhamira ya mashambulizi hayo na wala kutoa undani wa washukiwa wenyewe, lakini vyombo vya habari tayari viliyataja majina ya washukiwa kuwa ni ndugu wawili, Myles na Damien Sanderson, wenye umri wa miaka 30 na 31, ambao polisi ilisema walikimbia na gari.
Eneo la James Smith Cree Nation lenye wakaazi 2,500 lilitangaza hali ya hatari, huku wakaazi wengine wa jimbo la Saskatchewan wakitakiwa kusalia majumbani mwao.
Mauaji ya "kutisha"
Waziri Mkuu Justin Trudeau aliyaita mashambulizi hayo kuwa ya "kuogofya na kusikitisha", huku akitumia mtandao wa Twitter kutuma salamu za rambirambi na kuwataka raia kutii maagizo yanayotolewa na mamlaka zao wakati huu msako ukiendelea.
Picha za televisheni zilionesha nyumba chache katika maeneo ya mashambani katikati ya machaka ya majani na miti mirefu zikiwa zimezungushiwa utepe wa polisi, huku kwenye mitandao ya kijamii kukisambazwa picha za hali ilivyokuwa baada ya mashambulizi hayo.
Mmoja wa mashahidi wa tukio hilo, Diane Shier, aliliambia shirika la habari la Canada kwamba jirani yake aliyekuwa akiishi na mjukuu wake ni miongoni mwa waliouawa.
Katika miaka ya hivi karibuni, Canada imeshuhudia wimbi la mashambulizi ya watu silaha katika maeneo ya umma, jambo ambalo halikuwa likitajwa sana kwenye taifa hilo linalopakana na Marekani, iliyozowea mikasa ya aina hiyo.
Miongoni mwa matukio makubwa nchini Canada katika miaka ya karibuni ni afisa mmoja wa polisi kuwauwa watu 22 katika mji wa Nova Scotia, mwengine aliyewauwa waumini sita na kuwajeruhi watano katika msikiti mmoja mjini Quebec na dereva aliyewaponda wenda kwa miguu na kuwauwa 11 akiwajeruhi wengine 16 mjini Toronto.