wasafirishaji watu, marafiki hatari
4 Septemba 2015Ameongeza pia kwamba nchi hiyo inapaswa kutekeleza sheria za Umoja wa Ulaya kuhusu uhamiaji ikiwa ni pamoja na wahamiaji walioko katika makambi ya wazi katika kituo cha treni mashariki ya mji wa Budapest.
Wakati sakata hilo la wahamiaji likiendelea kwa upande mwingine limekuwa neema kubwa kwa wasafirishaji. Watu hawa hata hivyo ni lazima wapigwe vita, kwa kutumia jeshi la polisi na jeshi.
Waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban amesema wengi wa wahamiaji katika kituo hicho cha treni , ambao hawataki kuandikishwa nchini Hungary, wanataka kwenda Ujerumani, lakini amesema Hungary haiwezi kuwaruhusu kwenda kwa kuwa hali hiyo inahatarisha Austria kufunga mpaka wake.
Mtiririko wa wakimbizi haumaliziki
Mtiririko wa kuingia wakimbizi katika mataifa ya Ulaya haumaliziki na iwapo Umoja wa ulaya hautalinda mipaka yake , mamia kwa maelfu zaidi watamiminika, amesema waziri mkuu huyo. Kuna juhudi za kuzuwia wasafirishaji kuwaingiza wakimbizi katika mataifa ya Ulaya.
Na tarakimu pekee hazitoi picha kamili, lakini zinatoa picha ya kiwango kilichofikiwa. Idadi ya wakimbizi waliovuka mipaka na kuingia katika bara la Ulaya mwezi Juni pekee inafikia 107,500. Tarakimu hizi zimetolewa na shirika la Umoja wa Ulaya la ulinzi wa mipaka Frontex. Wengi wa watu hawa wametayarishiwa safari na makundi ya usafirishaji watu.
Idadi nyingine kubwa ya watu, wamepoteza maisha katika safari hizo, ambapo wakimbizi 71 walipoteza maisha nchini Austria mwishoni mwa mwezi Agosti, karibu wakimbizi 500 katika maboti mawili walikufa maji mwishoni mwa mwezi Agosti katika pwani ya Libya. Kiasi ya watu 800 walikufa wakiwa katika boti lililovunjika na kuzama mwezi Aprili karibu na kisiwa cha Lampedusa.
Wakimbizi wengi wamepoteza maisha
Kwa jumla kwa mujibu wa shirika la Umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR mwaka huu pekee zaidi ya wahamiaji 2,400 wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania wamefariki. Mtu angependa kujua , ni kiasi gani wasafirishaji wanapata , kutoka kwa watu hawa wenye shauku tu ya kuvuka bahari katika maboti mabovu na meli ndogo chakavu ama malori ambayo hayana hewa na kuhatarisha maisha yao.
Mtu anaweza tu kukadiria. Moja kati ya makadirio hayo yanatoka katika shirika la Umoja wa mataifa la kupambana na madawa ya kulevywa na uhalifu, UNODC. Shirika hilo linasema mapato ya jumla ya wasafirishaji watu yanafikia euro milioni 150 kwa mwaka.
Tarakimu hizo huenda zimepitwa na wakati hata hivyo. Hesabu hizo zinatokana na makadirio ya muda mrefu ambayo hayajafanyiwa mabadiliko kutoka jumla ya kiasi ya watu 55,000, ambao wanasafirishwa kila mwaka kuelekea bara la Ulaya. Makadirio ya shirika hilo la UNODC yakiangaliwa kwa msingi wa uingiaji wa wahamiaji katika mwezi wa Juni, inaweza kupanda na kufikia euro milioni 300 kama faida kwa wasafirishaji.
Soko la biashara hii ni kubwa
Ni soko kubwa . Na kama Tuesday Reitano kutoka shirika la Global Initiative againts Transnational organised crime , harakati za dunia kupambana na uhalifu wa kimataifa alivyosema , ni soko ambalo mtu anaweza kwa urahisi kuingia.
"Kupambana na uhalifu huu ni hali tata sana. Kwasababu , kwa kweli si soko lenye vikwazo vingi. Ni rahisi kwa watu hawa kujihusisha. Na hali hiyo iko sana Ufaransa, Uingereza, mzozo wa Calais, watu tu wa kawaida ambao wamekubali kuwapitisha wahamiaji mmoja ama wawili kwa kiasi cha zaidi ya pauni za Uingereza 1,000 kupitia njia ya chini ya bahari."
Reitano anasema katika mahojiano na DW kwamba wasafirishaji katika njia ya chini ya ardhi kutoka Ufaransa kwenda Uingereza, mtu mmoja hulazimika kulipa kiasi cha euro 1,500 ili aweze kuvushwa kutoka Calais nchini Ufaransa hadi Dover nchini Uingereza.
Ndio sababu mapambano dhidi ya biashara hii haramu ya kuwasafirisha watu ni sawa na mapambano dhidi ya nyoka mwenye vichwa vitatu. Kila ukipiga kimoja kingine kinajitokeza.
Mwandishi Matthias Hein / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Gakuba Daniel