1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Warusi wakimbia baada ya tangazo la uhamasishaji wa kijeshi

21 Septemba 2022

Idadi kubwa ya Warusi wamekimbia kuondoka nchini humo baada ya rais Vladmir Putin kuagiza kuwekwa tayari wanajeshi wa akiba 300,000 kusaidia katika vita vyake vya uvamizi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4HAPO
Russland Moskau | Fluginformation am Vnukovo International Airport
Picha: Vladimir Gerdo/TASS/dpa/picture alliance

Ndege zilijaa haraka na bei za tiketi zilizokuwa zimesalia zilipanda mara moja, kutokana na hofu kwamba mipaka ya Urusi ingefungwa wakati wowote au kutokea ukusanyaji mpana ambao unaweza kuwapeleka wanaume wengi wa Kirusi kupigana vita nchini Ukraine.

Tiketi za safari za ndege kutoka Moscow kwenda Belgrade zinazoendeshwa na shirika la ndege la Air Serbia, ambalo ndiyo shirika pekee la Ulaya mbali ya Turkish Airlines linaloendeleza safari za kwenda Urusi licha ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya, ziliuzwa kwa siku kadhaa zizajo.

Soam pia: Rais Putin atangaza uhamasishaji wa sehemu wa kijeshi Urusi

Gharama za safari kutoka Moscow hadi Istanbul au Dubai ziliongezeka ndani ya dakika chache kabla ya kupanda tena, na kufikia kiasi cha euro 9,200 kwa tiketi ya safari moja kwa daraja la kawaida.

Amri ya Putin inaainisha kuwa idadi ya watu watakaitwa kuhudumu jeshini itaamuliwa na wizara ya ulinzi. Waziri wa ulinzi Sergei Shoigu alisema katika mahojiano ya televisheni kwamba wanajeshi 300,000 wa akiba wenye uzoefu wa mapigano watakusanywa mwanzoni.

Urusi imeshuhudia idadi kubwa ya raia wake wakiondoka tangu Putin alipoamuru wanajeshi wake kuivamia Ukraine karibu miezi saba iliyopita.

Wakati wa hotuba yake kwa taifa mapema leo asubuhi, rais huyo alitangaza uhamasishaji wa sehemu wa kijeshi ili kupata wanajeshi wa akiba, huku akitoa kitisho kisicho cha wazi cha kutumia silaha za nyuklia dhidi ya maadui wa Urusi katika mataifa ya Magharibi.

"Nataka kuwakumbusha wale wanaoitishia Urusi kwamba nchi yetu ina aina mbalimbali za silaha za maangamizi, na baadhi za kisasa zaidi kuliko hata yalizo nazo mataifa ya NATO. Na endapo uhuru wa mipaka ya nchi yetu utatishiwa, bila shaka tutatumia njia zote zilizopo kwetu kuilinda Urusi na watu wake. Huu siyo mzaha," alisema Putin.

Marekani yasema inachukulia kwa uzito kitisho cha nyuklia

Msemaji wa Baraza la taifa la usalama la ikulu ya Marekani John Kirby, amesema Marekani inakichukulia kwa uzito kitisho hicho cha Putin, na kusema katika mahojiano na kutuo kimoja cha habari kwamba wanafuatilia kadiri wanavyoweza mikakati ya Urusi, na ikihitajika wao pia wanaweza kubadili ya kwao.

Russland | Wladimir Putin hält Rede an die Nation
Rais Putin akitangaza amri ya kuongeza idadi ya wanajeshi kwa ajili ya vita vya Ukraine.Picha: Russian Presidential Press and Information Office/Russian Look/picture alliance

Afisa mwingine wa Marekani amesema rais Joe Biden atatoa karipio kubwa dhidi ya Urusi katika hotuba yake leo kwa hadhira kuu ya Umoja wa Mataifa, kufuatia hatua ya Putin.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami NATO, Jens Stoltenberg, amesema tangazo la Putin halikuwa la kushangaza lakini litachochea zaidi mzozo huo ulioanza na uvamizi wa Urusi Februari 24.

Stoltenberg amesema hatua za Putin zinaonesha kuwa vita hiyo haiendi kulingana na mipango yake, na kwamba ni dhahiri rais huyo wa Urusi amaefanya kosa kubwa la kimahesabu.