1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Warundi wapiga kura ya maoni kuongeza utawala wa rais

Shisia Wasilwa
17 Mei 2018

Alhamisi Mei 17, raia wa Burundi wamepiga kura ya maoni kwa lengo la kuifanyia mageuzi katiba, ambapo pindi yakiidhinishwa, rais Pierre Nkurunziza  atakuwa na fursa ya kuongoza hadi mwaka 2034.

https://p.dw.com/p/2xtKA
Burundi Wahlen 2010
Picha: picture-alliance/dpa

Watu milioni tano wejiandikisha kushiriki kwenye kura hiyo ya maoni huku kukiwa na wasiwasi wa machafuko.

Polisi, wanajeshi kwenye magari yao walikuwa wakipiga doria nchini humo katika kura hiyo ya maoni inayojiri miaka mitatu baada ya Nkurunzinza kutaka kuongoza kwa muhula mwingine wa tatu, hatua iliyosababisha mzozo wa kisiasa ambao umesababisha watu 1,200 kufa na wengine 400,000 kulazimishwa kuyakimbia makaazi yao.

Mamia washiriki kura ya maoni

Mamia ya watu walipiga foleni kupiga kura ambapo wanaulizwa kuamua ndio ama  Hapana .

"Foleni ndefu zimeshuhudiwa wakati vituo vya kupigia kura vilipofunguliwa jijini Bujimbura. Warundi walikuwa wanasubiri kwa hamu na ghamu kupiga kura," msemaji wa rais Willy Nyamitwe aliandika kwenye mtandao wa  Twitter.

Mpiga picha wa shirika la habari la AFP pia alishuhudia foleni ndefu katika vituo vya kupigia kura kaskazini mwa Burundi.

"Naam nilikuja hapa kwa kuwa nilitaka kupiga kura ya 'ndio' kudhihirisha uhuru wa nchi yetu," alisema mkulima mmoja ambaye alitaja jina lake moja la Miburo, katika mji wa Ngozi.

Rais Pierre Nkurunzinza amepiga kura ya ndio Alhamisi asubuhi
Rais Pierre Nkurunzinza amepiga kura ya ndio Alhamisi asubuhiPicha: E. Ngendakumana

Nkurunziza, alipiga foleni kuanzia saa kumi na mbili asubuhi kupiga kura yake, huku akipongeza idadi kubwa ya watu waliojitokeza kufanya hivyo.  Mageuzi hayo yatatekelezwa iwapo zaidi ya asilimia 50 ya wapiga kura watapiga kura kuyaunga   mkono .

Upinzani wawataka wafuasi kupiga kura ya "la"

Huku wapinzani wengi wakiwa na hofu na wengine wakiwa uhamishoni, hapana shaka kuwa marekebisho hayo yatapitishwa, na kuwezesha Nkurunzinza mwenye umri wa miaka 54- ambaye amekuwa uongozini tangu mwaka 2005 kusalia madarakani kwa kipindi kingine cha miaka 16.

Kipindi cha kampeini kama tu kilichotangulia miaka mitatu iliyopita kiligubikwa na kukamatwa kamatwa kwa wapinzani, vitisho na mateso . Yamesema kutetea haki za binadamu .

Shirikisho la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu (FIDH) limesema, "kulikuwa na kampeini za kutia watu waswasi ili kuwalazimisha Warundi kupiga kura ya ndio."

Mtu mmoja ameliambia shirika la habari la AFP kuwa badhi ya maeneo katika mji mkuu na vijijini, kuwa wanachama wa kundi haramu la vijana wa Imbonerakure -- wanaohofiwa na kutuhumiwa na makundi ya kutetea haki za binadamu kwa maasi wakati wa mzozo kisiasa-- walikuwa wanalazimisha watu kupiga kura kwenye vituo.

Huku Muungano mkuu wa vyama vya upinzani ulioko uhamishoni CNARED ukiwataka watu kususia kura hiyo ya maoni, mpinzani mkuu wa Nkurunziza ndani ya Burundi, muasi wa zamani , kiongozi wa FNL Agathon Rwasa, amewataka wafuasi wake kupiga kura ya hapana.

Ni kosa kuwachochea watu wasishiriki

Agathon Rwasa kiongozi wa upinzani, Burundi
Agathon Rwasa kiongozi wa upinzani, Burundi Picha: E. Ngendakumana

Tangazo la rais mapema mwezi huu limesema kuwa yeyote anayewashauri watu kususia uchaguzi anakabiliwa na hatari ya kufungwa hadi miaka mitatu gerezani.

Hakuna waangalizi wa kimataifa katika  kura hiyo ya maoni na wengi wa waandishi habari wa kigeni hawakuruhusiwa kuingia nchini humo kutokana na vizuizi vya utawala nchini humo.

Kwa wengi kura hiyo ya maoni ni pigo kwa matumaini ya amani ya kudumu katika taifa ambalo demokarasia yake inasuasua na kukabiliwa na mzozo wa kisiasa wa muda mrefu kati ya Wahutu walio wengi na Watutsi ambao wameshikilia madaraka kwa muda mrefu.

Hussein Radjabu ni mmoja wa wapinzani ambao wakati mmoja alikuwa mshirika wa karibu wa Nkurunziza na aliwekwa gerezani kwasababu ya uhaini lakini akaitoroka nchi hiyo. Akizungumza na kutoka uhamishoni na a shirika la Associated Press alisema "njia iliyoko sasa ni kutumia bunduki na kwamba wamejitolea kutumia mbinu zote kufanikisha malengo yao."

Mwandishi: Shisia Wasilwa Ap, Afp, Afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman