1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Warithi wa Merkel watofautiana kuhusu China, Urusi

19 Mei 2021

Wagombea wawili wanaowania kumrithi kansela wa Ujerumani Angela Merkel wanakinzana kuhusu dhima ya Ujerumani katika masuala ya dunia, kati ya mwendelezo na msimamo wa kujiamini zaidi, hasa kuhusiana na China na Urusi.

https://p.dw.com/p/3tdI4
Die Kanzlerkandidaten von CDU CSU und Buendnis90/dieGruenen zur Bundestagswahl 2021.
Picha: Malte Ossowski/SVEN SIMON/picture alliance

Muungano wa wahafidhina wa Merkel na mgombea wao Armin Laschet, mwenye umri wa miaka 60, mpinzani wake kutoka chama cha Kijani, Annalena Baerbock mwenye umri wa miaka 40, wanakabana koo katika uchunguzi wa maoni ya wapigakura, ikiwa imesalia miezi minne kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu ambao utaashiria mwisho wa enzi ya kansela huyo wa muda mrefu. 

Wote wawili wana uzoefu mdogo katika siasa za ulimwengu.

Laschet alikuwa mjumbe wa bunge la Ulaya mwanzoni mwa miaka ya 2000 na sasa anaongoza jimbo lenye wakaazi wengi zaidi nchini Ujerumani la North Rheine Westphalia. Baerbock wakati huo, alihudumu kama masaidizi wa mbunge wa Ulaya kupitia chama cha Kijani kuanzia 2005 hadi 2008, na ana shahada ya sheria ya kimataifa kutoka shule ya uchumi ya London.

Infografik Deutschlandtrend Direktwahl BundeskanzlerIn
Uchunguzi wa maoni ya wapigakura wa Infratest/ARD wa Mei 6, 2021, ulimuweka mbele mgombea wa chama cha Kijani Annalena Baerbock kwa asilimia 28 dhidi ya wapinzania wake, Armin Laschet wa CDU/CSU na Olaf Scholz wa SPD.

Wote wawili wamezungumzia utayari wao kuegemea upande wa Marekani na ahadi yao kwa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami NATO. Lakini yanapokuja masuala kuhusu China na Urusi, wawili hao wanatofautiana vikali.

Wachambuzi wanabainisha kwamba wakati Laschet anatazamwa sana kama mgombea mwenye uwezekano wa kuendeleza msimamo wa kidiplomasia wa Merkel, Baerbock anaweza kuleta mabadiliko katika sauti inapokuja kwenye masuala kuhusu Beijing na Moscow.

Soma pia:Annalena Baerbock mgombea ukansela wa chama cha Kijani 

Merkel mara zote amechukuwa msimamo yakinifu kuhusu Urusi na China, akihoji kuwa inawezekana kutafuta maslahi ya pamoja na kuendelea kufanya biashara na mataifa hayo wakati huo huo ukizungumzia tofauti kwenye masuala kama haki za binadamu.

Lakini wakosoaji wamemtuhumu kwa kukosa makali mbele ya Vladmir Putin au Xi Jinping wakati akijaribu kulinda maslahi ya kibiashara ya Ujerumani.

Deutschland Germany`s Next Merkel
Wagombea wakuu wa vyama katika uchaguzi wa Septemba nchini Ujerumani, Annalena Baerbock wa chama cha Kijani, Armin Laschet wa muungano wa CDU/CSU na Olaf Scholz wa SPD.Picha: Leonie von Hammerstein/DW

Utetezi wake wa mradi tata wa bomba la gesi la Nord Stream 2 kati ya Urusi na Ujerumani uliwakasirisha hata washirika.

Na licha ya mizozo inayoongezeka na Moscow kuhusu masuala yakiwemo utwaaji wa kimabavu wa rasi ya Crimea au kulishwa sumu kwa mwanasiasa wa upinzani Alexei Navalny, Merkel ameshikilia kuendeleza mradi wa bomba hilo wenye thamani ya euro bilioni 10.

Mkakato tofauti kwa tawala za kimabavu

Baerbock anataka bomba hilo kusitishwa, akisema linadhoofisha vikwazo dhidi ya Urusi na kutoa kitisho kwa mazingira. Katika mahojiano ya karibuni na gazeti la kila siku la Frankfurter Allgemeine mnamo mwezi Aprili, Baerbock alisema anaunga mkono mkakati tofauti wa ushirikiano na tawala za kimabavu.

Soma pia: Maoni: Manifesto ya AfD ni hatari kwa Ujerumani

Kwa upande wake, Laschet ambaye ameelezwa na baadhi mjini Moscow kama mhurumiaji, amesema serikali inafuata mkondo sahihi kuhusu bomba la Nord Stream. Mnamo mwaka 2018, alikosolewa kwa kuhoji iwapo Uingereza ilikuwa na ushahidi kwamba Urusi ilihusika na kupewa sumu Sergei Skripal, ingawa baadae alibadili msimamo.

Armin Laschet Annalena Baerbock  MSC München Sicherheitskonferenz
Armin Laschet na Annalena Baerbock wakishiriki mjadala wa kamati wakati wa mkutano wa usalama wa Munich, Februari 16, 2020.Picha: Getty Images/C. Stache

Kama Merkel, Laschet hajakuwa muoga kuikosoa Urusi na ametoa wito wa kuachiwa kwa Navalny, lakini pia alisema anaamini mradi wa Nord Stream unapaswa kuwa huru na hilo.

Vile vile kuhusu China, Laschet anatarajiwa kuendeleza mkondo wa Merkel, ambaye alikuwa msitari wa mbele wa kujadiliana makubaliano ya uwekezaji kati ya Beijing na Umoja wa Ulaya mwishoni mwa 2020, na amekuwa akiimarisha uhusiano wa kibiashara na China kwa miaka kadhaa sasa.

Katika mahojiano na gazeti la Frankfurter Allgemeine, Laschet alisema kinachoendelea kwa wa Uighur nchini China hakikubaliki.

Soma pia: Maoni: Wahafidhina wa CDU njia panda

Baerbock ameonesha msimamo mkali zaidi kuhusu namna China inavyowatendea wa Uighur. Wakati alikiri kwamba siyo haki za binadamu upande mmoja na maslahi ya kiuchumi upande mwingine, alisema Ulaya inaweza kukataa kununua bidhaa zozote zilizotengenezwa katika mikoa ambako ukiukaji unatendeka, kwa mfano Xinjiang.

Alidai mwezi Aprili kwamba Umoja wa Ulaya haujashughulikia ipasavyo masuala ya ufanyishwaji kazi wa laazima kwa jami ya Uinghur inayokandamizwa, katika muktadha wa makubaliano ya uwekezaji kati ya Umoja huo na China, ambayo yalisitishwa mwanzoni mwa mwezi Mei.

Akidokeza namna anavyopanga kulaazimisha msimamo wake dhidi ya wadau wa kimataifa, Baerbock alisema katika mahojiano na shirika la habari la RND, kwamba haitoshi kupiga tu meza,na kuongeza kuwa mtu anahitaji kuwa na msimamo wa wazi, na dira yake mwenyewe, ili kutumia kikamilifu uwanja mzima wa diplomasia, ambao unahusisha majadiliano, vivutio na ukali.

Chanzo: AFP