1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani Syria wakutana Riyadh

Admin.WagnerD9 Desemba 2015

Wawakilishi wa makundi ya upinzani nchini Syria yameanza mazungumzo yanayodhaminiwa na Saudi Arabia, yenye lengo la kusaka msimamo mmoja katika mazungumzo yanayotarajiwa baina yao na utawala wa rais Bashar al-Assad.

https://p.dw.com/p/1HKmN
Waasi wa Syria katika mikutano ya siku za nyuma
Waasi wa Syria katika mikutano ya siku za nyumaPicha: Getty Images/AFP/K. Desouki

Ingawa makundi yote ya upinzani hayakualikwa katika mkutano huo unaofanyika mjini Riyadh, ni mara ya kwanza kwa makundi mengi ya kisiasa na kijeshi kukaa pamoja tangu kuanza kwa mzozo wa Syria mwaka 2011.

Lengo kuu la mkutano huo unaohudhuriwa na wajumbe 100 ni kuweka kundi moja litakalowakilisha wapinzani wote katika mkutano na serikali ya Assad, ambao nchi zenye nguvu duniani zinaamini utafanyika kabla ya mwaka huu kumalizika.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Saudi Arabia Adel al Jubeir ambaye ameonya mara kadhaa kwamba ikiwa rais Assad hataki kuachia madaraka kwa amani anaweza kulazimishwa kijeshi kufanya hivyo, amehudhuria mkutano huo kwa muda mfupi kuwakaribisha wajumbe na kuwatakia mafanikio.

Baadhi ya wapinzani wenye silaha pia wamealikwa katika mkutano wa Riyadh
Baadhi ya wapinzani wenye silaha pia wamealikwa katika mkutano wa RiyadhPicha: Reuters/O. Sanadiki

Msimamo mmoja miongoni mwa wapinzani

Mwenyekiti wa muungano wa wapinzani wa Syria Khaled Khoja amesema makundi mengi yaliyowakilishwa yana maoni sawa.

''Makundi mengi ya upinzani yaliyoundwa nchini Misri, Dubai na nchi nyingine , yamewasilishwa na kamati zao'' amesema Khoja, na kuongeza kuwa kumekuwepo mawasiliano, na mengi ya makundi hayo yanakubaliana kuhusu mtazamo wa kisiasa juu ya mchakato wa kipindi cha mpito, na hivyo maoni yetu ni kwamba njia mwafaka ni kupata maafikiano.''

Mkutano huo ambao unafanyika katika hoteli ya kifahari yenye ulinzi mkali, na unaongoza na Abdulaziz Sager, msaudia ambaye pia ni mwenyekiti wa kituo cha utafiti cha Ghuba ambacho kiko mjini Geneva. Shirika la habari la Saudi Arabia limesema kuwa mkutano huo pia umeitikiwa na makundi mengi ya upinzani kutoka ndani ya Syria.

Mada ngumu kwenye mazungumzo

Kulingana na ratiba ya mazungumzo, siku ya kwanza imejikita juu ya sura ambayo muafaka wa kisiasa inaweza kupewa, na siku ya pili, kesho Alhamis, wajumbe watajadili tatizo la ugaidi, usitishaji mapigano na mchakato wa kuijenga upya Syria.

Kuikarabati upya Syria ni mojawapo ya masuala muhimu yatakayojadiliwa katika mkutano huo
Kuikarabati upya Syria ni mojawapo ya masuala muhimu yatakayojadiliwa katika mkutano huoPicha: picture-alliance/AP Photo

Khoja ambaye muungano anaouongoza wa National Coalition una makao yake mjini Istanbul, amesema anayo matumaini kwamba mkutano huo utafanikiwa kuunda kundi moja la uwakilishi katika mazungumzo, na pia juu ya nguzo kuu za mazungumzo baina yao na serikali ya Rais Bashar al Assad.

Makundi yenye silaha yanayoaminika kuwa ya kigaini, kama vile Dola la Kiislamu, na al-Nusra Front hayakualikwa katika mazungumzo hayo ya mjini Riyadh, lakini washirika wa al-Nusra, Ahrar al-Sham wamethibitisha kushiriki kwao, hali ambayo imeyafanya baadhi ya makundi mengine kujiondoa katika mazungumzo hayo.

Kundi jingine ambalo limetengwa katika mazungumzo hayo ni lile la Syrian Democratic Forces linaloungwa mkono na Marekani, ambalo linawajumuisha wakurdi, wasuni na wakristo wanaolipinga kundi la IS.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri: Mohammed Khelef