Mapigano yashika kasi Somalia
1 Machi 2019Milipuko na milio ya risasi ilisikika usiku kucha mjini Mogadishu huku askari wakisema hadi kufikia Ijumaa asubuhi, idadi ya watu waliokufa ilikaribia watu 30 na majeruhi 80 waliripotiwa kupelekwa katika hospitali mbalimbali. Idadi ya vifo ilitarajiwa kuongezeka kutokana na mapambano yaliyokuwa yakiendelea katika eneo la hoteli hiyo iliyozungukwa na maduka, migahawa na hoteli nyingine.
Afisa wa polisi Meja Mohammed Hussein aliliambia shirika la habari la Reuters siku ya Ijumaa kwamba vikosi vya polisi viliwaokoa raia wengine waliokuwa kwenye hoteli na majengo jirani. Aliongeza kusema wanamgambo wa Al shabaab bado walikuwa wamenasa ndani ya hoteli huku makabiliano ya risasi yakiendelea.
Afisa huyo alisema ilikuwa vigumu kwa vikosi vya ulinzi kuingia kwenye jengo la hoteli walimokuwamo wanamgambo hao Alhamisi usiku kwa sababu ya giza baada ya umeme kukatika kutokana na mlipuko wa bomu. Afisa huyo alieleza matumaini ya kumalizika kwa operesheni hiyo ya kuwakamata wanamgambo hao na kuwaokoa raia wengine baada ya mapambazuko.
Kundi la Al Shabaab kupitia msemaji wake lilinukuliwa likisema ingawa vikosi vya serikali vilijaribu kuingia eneo la Al Mukaram mara tatu bado kundi lake lilikuwa likiidhibiti hoteli hiyo wakati barabara kuu ya kuingia eneo la hoteli hiyo ikifungwa kwa sababu za kiusalama. Hoteli hiyo ya Al Mukaram hutumiwa na viongozi wa serikali ya Somalia na imekuwa ikilengwa mara kwa mara na wanamgambo wa Al Shabaab.
Raia wakumbwa na hofu kuwatafuta ndugu zao
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo walionekana wakiwa wamechanganyikiwa na kupiga simu kila wakati wakiwatafuta ndugu zao.
Bi Halima Oma, ambaye ni mama wa watoto wa tatu, amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema, "Nimekuwa nikikimbia huku na kule kutoka kwenye eneo ulipotokea mlipuko tangu jana jioni nikimtafuta mume na kaka yangu ambao walikuwa wanauza katika duka eneo ulipotokea mlipuko. Nimewaona hospitali na wako kwenye hali mbaya. Mume wangu ameumizwa tumboni na kaka amepata majeraha kwenye mikono yote miwili.''
Somalia imekuwa ikikabiliwa na vitendo vya uvunjaji sheria na vurugu tangu mwaka 1991. Kundi la Al Shabaab linalohushishwa na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda linapigana kuipinga serikali inayoungwa mkono na nchi za magharibi na kulindwa na vikosi vya tume ya kulinda amani vya Umoja wa Afrika. Wanamgambo wa Al Shabaab pia wamekuwa wakikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa vikosi vya Marekani ambapo mara kadhaa, ikiwemo mwanzoni mwa mwaka huu, Marekani ilifanikiwa kuwaua wanamgambo hamsini na watano.
(RTRE/AP)