Wapalestina waukimbia mji wa Rafah
8 Mei 2024Licha ya mayowe kutoka kwa jamii ya kimataifa kupinga mashambulio hayo ya ardhini, Israel ilipeleka vifaru vyake katika mji wa Rafah hapo jana Jumanne na wanajeshi wake wakakiteka kivuko kinachounganisha mji wa Rafah na Misri ambacho ni njia kuu ya kupitishia misaada kwenda katika eneo lililozingirwa la Palestina.
Soma Pia: Guterres asema kushambulia Rafah itakuwa janga la kibinadamu
Ikulu ya Marekani imelaani kukatizwa kwa zoezi la utoaji wa misaada, huku afisa mmoja mkuu wa nchi hiyo akifichua kwamba Washington ilisitisha kuipelekea Israel shehena ya mabomu wiki iliyopita.
Hatua hiyo ilijiri baada ya mshirika wake huyo kushindwa kuihakikishia Marekani kwamba haitoendelea na mipango yake ya kufanya mashambulizi ya ardhini katika mji wa Rafah.
Hata hivyo, saa chache baadae jeshi la Israel lilitangaza kwamba linakifungua tena kivuko cha Kerem Shalom, na kile cha Erez kwa ajili kuingizwa msaada mkubwa katika Ukanda wa Gaza.
Lakini licha ya kauli hiyo ya Israel, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, limesema kivuko cha Kerem Shalom ambacho Israel ilikifunga baada ya wanajeshi wake wanne kuuawa katika shambulio la roketi mnamo siku ya Jumapili bado hakijafunguliwa.
Mashambulizi makubwa usiku wa kuamkia Jumatano
Eneo hilo la Rafah lilishuhudia mashambulizi makubwa katika usiku wa kuamkia Jumatano na picha za televisheni za shirika la habari la AFP ziliwaonyesha Wapalestina waliokuwa wakihangaika gizani kuwaokoa wapendwa wao kutoka chini ya vifusi kwenye jengo moja lililoshambuliwa katika mji huo.
Soma Pia: Biden amuonya Netanyahu operesheni ya ardhini mji wa Rafah
Wakati mapigano yakiendelea kwenye viunga vya mji wa Rafah leo hii Jumatano huku wanajeshi wa Israel wakiendelea kuingia katika mji huo, Wapalestina wameingia tena kwenye harakati za kutafuta pa kwenda wakiviacha vitongoji vya eneo la kusini mwa mji wa Gaza.
Israel imetishia kufanya mashambulizi makubwa katika mji wa Rafah ikidai kuwa inataka kuwaangamiza maelfu ya wapiganaji wa Hamas ambao imesema wamejificha kwenye mji huo unaowahifadhi zaidi ya watu milioni moja.
Jeshi la Israel limesema linaendesha kile linachokiita "operesheni makhsusi" huko Rafah inayolenga kuwamaliza wanamgambo wa Hamas na kuiangamiza miundombinu inayotumiwa na kundi hilo linaloendesha Ukanda wa Gaza.
Jeshi la Israel limewataka raia wa Palestina waende kwenye eneo salama lililotengwa umbali wa takribani kilomita 20 kutoka Rafah.
Wapalestina milioni 1.4 wamekuwa wakijihifadhi katika mji huo wa Rafah, na hali hiyo ya kutakiwa kuondoka inaleta hofu ya kuongezeka vifo na watu kujeruhiwa.
Soma Pia: Israel yawaamuru maelfu ya Wapalestina kuondoka Rafah
Vita hivyo vilianza tarehe 7 Oktoba mwaka jana wakati wanamgambo wa Hamas walipovuka na kuingia Israel kutoka Gaza. Kwenye mashambulizi yao watu wapatao 1,200 waliuliwa na wengine zaidi ya 200 walichukuliwa mateka kulingana na takwimu za Israel.
Vyanzo: AFP/RTRE