1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina waukataa uamuzi wa Mahakama ya Israel

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
3 Agosti 2021

Mahakama Kuu ya Israel imetoa pendekezo juu ya kesi inayohusu kutimuliwa kwa wapalestina kutoka kwenye kitongoji cha Sheikh Jarrah katika mji wa Jerusalem Mashariki. Hata hivyo wapalestina wamelikataa pendekezo hilo.

https://p.dw.com/p/3yTxZ
Jerusalem | Sheik Jarrah | Al Kurd
Picha: Tania Kraemer/DW

Wapalestina wanaotishiwa kutimuliwa kutoka mji wa Jerusalem Mashariki wameukataa uamuzi wa mahakama kuu ya Israel wa kuwataka wapalestina hao wawe wapangaji kwenye nyumba za shirika la nyumba la walowezi wa kiyahudi. Mahakama hiyo ilitoa mapendekezo kadhaa kwa familia nne za wapalestina hao wanaoishi kwenye kitongoji cha Sheikh Jarrah, ikiwa pamoja na haki ya kuendelea kuishi kwenye nyumba zao wakiwa na hadhi ya kulindwa kisheria bila ya hofu ya kufukuzwa katika miaka ijayo. Hata hivyo wapalestina wameupinga uamuzi huo.

Baadhi ya maeneo ya kitongoji cha Sheikh Jarrah
Baadhi ya maeneo ya kitongoji cha Sheikh Jarrah Picha: Taina Kraemer/DW

Mkaazi mmoja wa Sheikh Jarrah Mohammed El-Kurd, ameeleza kuwa Mahakama Kuu ya Israel imekwepa kubeba dhima ya kutoa uamuzi. Badala yake imesuasua na kuwapachika wao shinikizo kubwa la kufanya uamuzi juu ya kufikia mapatano na mashirika ya walowezi. Amesema ukweli ni kwamba hawatalipa kodi kwa watu wasiokuwa na haki ya kumiliki nyumba zao. El Kurd amesema hali imeendelea kuwa hivyo kwa miaka 49 iliyopita ya njama za kuchelewesha na kuahirisha uamuzi. Mkaazi huyo bwana Mohammed el- Kurd amesema njama hizo hazitafanya kazi tena. Ameeleza kuwa mfumo huo umetokana na uporaji wa ardhi na kukandamizwa kwa wapalestina. Amesema mfumo huo hauwezi kutoa haki kwa wapalestina.

Kesi zilizosikilizwa kwenye mahakama kuu ya Israel zinawahusu wapalestina 70 wanaotishiwa kufukuzwa na walowezi wa kiyahudi kutoka kwenye maskani yao. Mahakama za ngazi za chini hapo awali ziliridhia hatua ya kufukuzwa kwa wapalestina hao. Mahakama hizo zilisema wapalestina hao wamejenga nyumba zao kwenye maeneo yaliyokuwa yanamilikuwa na wayahudi kabla hata ya kuundwa kwa nchi ya Israel mnamo mwaka 1948.

Wapalestina walioandamana kupinga hatua ya kuondolewa kwa nguvu kutoka kwenye kitongoji cha Sheikh Jarrah.
Wapalestina walioandamana kupinga hatua ya kuondolewa kwa nguvu kutoka kwenye kitongoji cha Sheikh Jarrah. Picha: Laith Al-jnaidi /AA/picture alliance

Mzozo huo ndio uliosababisha vita vya siku 11 mnamo mwezi Mei kati ya Israel na wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Hata hivyo mahakama kuu ya Israel imetoa uamuzi wa mwafaka. Mahakama hiyo imetoa uamuzi wa kuwalinda wapalestina dhidi ya kufukuzwa kwenye makazi yao lakini haikutatua suala la umiliki wa ardhi.

Wapalestina hao wa kitongoji cha Sheikh Jarrah katika mji wa Jerusalem Mashariki wamesema hawatatambua  umiliki wa walowezi wa kiyahudi. Mkaazi mwengine wa kitongoji hicho amesema, kwa mtazamao wake hakuna uamuzi uliofikiwa mpaka sasa.

Vyanzo:/AFP/AP/  https://p.dw.com/p/3yS5m