Wapalestina wakubaliana kuunda serikali ya Umoja wa kitaifa
23 Julai 2024Makundi mbali mbali ya Palestina ikiwemo Hamas na chama cha Fatah wamekubaliana kumaliza tofauti zao na kuunda serikali ya Umoja wa kitaifa.
Makubaliano ya kile kilichoitwa azimio la Beijing, yametokana na mazungumzo ya kutafuta maridhiano yaliyoanza tangu tarehe 21 mwezi huu wa Julai na yaliyomalizika leo Jumanne na kutiwa saini katika sherehe iliyofanyika Beijing.
Makundi 14 ya Palestina yameshiriki na kusaini makubaliano hayo ikiwemo chama cha Fatah na Hamas. Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi aliyesimamia mchakato huo wa maridhiano ya Wapestina amefafanua lengo la azimio hilo la Beijing.
''Maridhiano muhimu ya mazungumzo haya ya Beijing miongoni mwa makundi ya Wapalestina ni ahadi ya kutekeleza maridhiano na umoja wa kitaifa kwa makundi yote 14. Kilichoko wazi ni kwamba chama cha ukombozi wa Wapalestina PLO ndio chama pekee mwakilishi halali wa umma wa Wapalestina. Jambo muhimu zaidi ni makubaliano yaliyofikiwa ya kuunda serikali ya mpito ya maridhiano ya kitaifa itakayotawala Ukanda wa Gaza baada ya Vita.''
Uhasama wa Fatah na Hamas ni wa miaka mingi
Kwa miaka 17, makundi ya Palestina yamekuwa kwenye mivutano. Mpaka wakati huu eneo la Ukanda wa Gaza limekuwa likitawaliwa na kundi la Hamas peke yake.
Hata hivyo Kiongozi mmoja mwandamizi wa kundi hilo aliyeshiriki mazungumzo ya Beijing Hussam Badran amesema jambo muhimu kwenye azimio la Beijing ni kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambayo sio tu itaiongoza Gaza bali pia itayashughulikia masuala yote ya Wapalestina, ,kuanzia Gaza hadi Ukingo wa Magharibi.
Itasimamia Ujenzi wa Palestina pamoja na kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi.
Israel tayari imeshakikosoa chama cha rais Mahmoud Abbas cha Fatah kwa kuingia makubaliano hayo pamoja na Hamas.Soma pia: Netanyahu aanza ziara nchini Marekani
Lengo kubwa la Waziri mkuu wa Israel la kuendeleza vita Ukanda wa Gaza, amekuwa akisisitiza ni kuliangamiza kabisa kundi la Hamas linaloungwa mkono na Iran na amekuwa akipinga kabisa kundi hilo kupewa dhima yoyote katika serikali itakayoundwa Gaza baada ya vita.
Je hatua ya China ni mapinduzi ya kidiplomasia Mashariki ya Kati?
Kufikiwa kwa makubaliano hayo ya Beijing kunamaanisha, China imefanikiwa kufanya mapinduzi ya kidiplomasia na kuongeza ushawishi wake katika eneo la Mashariki ya kati, na hasa baada ya kufanikiwa pia kuleta maelewano mwaka jana kati ya mahasimu wa miaka Saudi Arabia na Iran.
Azimio hilo la Beijing limekuja wakati muhimu kabisa kwa Wapalestina ambao wanaendelea kushuhudia mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.Soma pia: Wapalestina watano wauawa kwa droni katika Ukingo wa Magharibi
Taarifa za vyombo vya habari za hivi punde zinasema, Wapalestina watano wameuwawa katika shambulio la droni lililofanywa na Israel katika mji wa Tulkarm, Ukingo wa Magharibi.
Lakini kwa upande mwingine ofisi ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu imesema kiongozi huyo wa Israel ameziarifu familia za mateka wanaoshikiliwa Gaza, kwamba makubaliano yatakayofanikisha wapendwa wao kuachiliwa huru huenda yanakaribia kufikiwa.
Netanyahu alizungumza na familia hizo jana Jumatatu mjini Washington ambako anatarajiwa kukutana baadae wiki hii na rais Joe Biden na pia kulihutubia bunge la Marekani.