1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina kuandamana kuipinga Marekani kuhusu Jerusalem

8 Desemba 2017

Wapalestina watarajiwa kuandamana kwa wingi baada ya sala ya Ijumaa katika Ukingo wa Magharibi kusini mwa Jerusalem na katika Ukanda wa Gaza kulaani tangazo la Trump la kuutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel

https://p.dw.com/p/2p08h
Bethlehem Proteste gegen Anerkennung USA Jerusalem
Picha: picture-alliance/AA/M. Wazwaz

Wapalestina wenye hasira wameitisha siku ya ghadhabu leo Ijumaa wakati maandamano ya kupinga hatua ya rais wa Marekani Donald Trump kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel yakisambaa. Wakati huohuo afisa mkuu wa Palestina amesema kuwa makamu wa rais wa Marekani Mike Pence hakaribishwi kufuatia mabadiliko hayo ya sera kuhusu Jerusalem

Wapalestina leo wanatarajiwa kuandamana kwa wingi baada ya sala ya Ijumaa katika Ukingo wa Magharibi kusini mwa Jerusalem na katika Ukanda wa Gaza kulaani tangazo la Trump la kuutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.

Maandamano katika nchi za Kiislamu

Maandamano hayo pia yanatarajiwa kufanyika eneo zima la Mashariki ya Kati na mataifa ya Kiislamu. Nchini Malaysia tayari zaidi ya Waislamu 1,000 wameandamana nje ya ubalozi wa Marekani mjini Kuala Lumpur.

Msemaji wa polisi wa Israel Micky Rosenfeld amesema maafisa wa usalama wa Israel wamepelekwa kushika doria na wako tayari kukabiliana na maandamano yoyote ambayo yatafanyika kinyume cha sheria.

Maafisa wa polisi wa Israel wakikabili waandamanaji wanaopinga tangazo la Rais Trump kuhusu Jerusalem
Maafisa wa polisi wa Israel wakikabili waandamanaji wanaopinga tangazo la Rais Trump kuhusu JerusalemPicha: picture-alliance/AA/M. Wazwaz

"Polisi ya Israel na vikosi vyake viko katika mitaa ya Jerusalem na maeneo jirani na pia katika kivuko cha Qalandiya. Vikosi hivyo vitashughulikia maandamano yoyote ambayo si halali ikiwa yatatokea sehemu yoyote ya Jerusalem. Tunatumai hali itakuwa tulivu lakini tutaikabili hali kwa dharura haja ikitokea katika mji wa Kale au katika maeneo jirani ya Kiarabu kuhusu maandamano yasiyo ya kisheria"

Makabiliano kati ya Wapalestina na Israel

Siku ya Alhamisi, mapigano yalizuka kati ya Wapalestina na vikosi vya Israel na kuilazimu Israel kuwapeleka mamia ya maafisa zaidi wa usalama katika Ukingo wa Magharibi.  Wapalestina 22  walijeruhiwa kutokana na mashambulizi ya Israel. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la Hilali nyekundu.

Kwenye hotuba iliyotolewa katika mji wa Gaza, kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh alitowa mwito wa kuanzishwa harakati mpya za uasi na mapmbano au Intifada dhidi ya  Israel.  Baada ya saa chache, makombora kadhaa yalirushwa kutoka Ukanda wa Gaza. Jeshi la Israel limesema hayo na kuongeza kuwa kombora moja lilipiga eneo la Israel na kulazimisha majeshi ya Israel kulipiza kisasi kwa kulenga maeneo mawili ya Gaza huku ikilaumu Hamas.

Waandamanaji wakibeba mabango yanayolishutumu tangazo la Donald Trump kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel
Waandamanaji wakibeba mabango yanayolishutumu tangazo la Donald Trump kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa IsraelPicha: picture-alliance/AA/I. Rimawi

Mike Pence hakaribishwi Palestina

Wakati huohuo afisa mmoja mkuu wa Palestina amesema makamu wa rais wa Marekani Mike Pence aliyetarajiwa kuzuru Palestina kukutana na rais wa Wapalestina Mahmud Abbas hakaribishwi kufuatia mabadiliko ya sera ambayo yamemaliza miongo kadhaa ya ukosefu wa maelewano kuhusu mji unaozozaniwa wa Jerusalem. Ikulu ya Marekani imesema itakuwa vyema kuufuta mkutano huo uliotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Palestina imeliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuubatilisha uamuzi wa Trump. Baraza la Hamas limeitisha mkutano wa dharura leo kuhusu mzozo wa Jerusalem.

Tangazo la rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Jerusalem limekosolewa takriban ulimwenguni kote. Lakini waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amemsifia Trump na kusema jina lake litahusishwa na historia ndefu ya Jerusalem. Amezihimiza nchi nyingine pia kufuata mkondo huo

Mwandishi: John Juma/APE/AFPE

Mhariri: Yusuf Saumu