1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaume wa Afrika wanavyobadili imani

Mohamed Dahman27 Novemba 2012

Ingawa baadhi ya mila za Kiafrika zinataka mwanaume awe na watoto wengi na wa kiume kama mrithi, wanaume wa Afrika wameanza kubadilika kwa kuachana na mila hizo baada ya kutambua umuhimu wa uzazi wa majira.

https://p.dw.com/p/16mT4
Arbeitslose afrikanische Männer sitzen auf einer Mauer, Germa, Libyen
Wanaume wa KiafrikaPicha: picture-alliance/dpa

Uganda ni mojawapo ya nchi zenye idadi kubwa la ongezeko la watu ambapo huongezeka kwa asilimia 3.2 kwa mwaka. Idadi ya watu wa nchi hiyo hivi sasa imefikia milioni 34.

Anthony Bugembe afisa mipango katika Sekreteriati ya Idadi ya Watu kwenye Wizara ya Fedha ameliambia shirika la habari la IPS kwamba watu milioni moja huongezeka katika idadi ya watu wa Uganda kila mwaka lakini rasilmali haziongezeki kulingana na kiwango hicho.

Charles Kayongo ni miongoni mwa kizazi kinachoinukia cha waume vijana nchini Uganda ambao wameanza kukaidi mila ya Kiafrika ya kuzaa watoto wengi na badala yake kuwa na familia ndogo wanazoweza kuzimudu.

Kayongo ni baba wa wasichana wawili wenye umri wa miaka mitano na miaka miwili.Na juu ya kwamba mila za muda mrefu katika kabila lake la Baganda zinasema mwanaume anapaswa kuwa na watoto wengi na mtoto wa kiume kama mrithi Kayongo anakataa kuwa na watoto zaidi.Kama vile walivyo wazazi wengine vijana wanaokabiliwa na ukata wa fedha katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki ambao wanatamani kuwa na maisha ya kisasa anasema kwamba yeye na mke wake Eunice Kayongo wanataka kuwa na familia ndogo.

Black school children with a white boy eating an ice cream cone in front of them, Johannesburg, South Africa.
Watoto barani Afrika

Kayongo mwenye umri wa 33 ameliambia shirika la habari la IPS akiwa nyumbani kwake huko Mukono kwenye viunga vya mji mkuu wa Kampala kwamba inatosha,hataki kuwa na watoto zaidi na kwamba amelijadili hilo na mke wake na wamekuwa wakitumia vidonge na kondomu kwa miaka miwili iliopita. Amesema Gharama za chakula,kuwapeleka watoto shule na kununuwa madawa tayari zimemuelemea.

Kayongo ambaye anamiliki kilabu cha pombe anasema anatumia dola kumi kwa siku kwa ajili ya familia yake na kwamba anapata dola 440 kwa mwezi.

Lynda Birungi kutoka Kundi la Afya ya Uzazi lilioko katika Mpango wa Taifa wa Uzazi wa Majira nchini Uganda anasema akina baba wengi vijana wamekuwa wakijihusisha katika uzazi wa majira kuliko ilivyokuwa hapo zamani.Katika kila kundi la wanawake watano wanaokwenda kwenye zanahati zao ni mmoja tu anakwenda na mwanaume,lakini miaka ishirini iliopita wanaume walikuwa hawendi kabisa.

Katika taifa la kusini mwa Afrika la Malawi kile kilichoanza miaka 11 uliopita kama ujumbe wa maafisa 10 wa polisi kufanya safari za kuhubiri dhidi ya ukatili wa majumbani wenye kuchochea mimba zisizohitajika na kuongeza vifo vya uzazi limegeuka kuwa vuguvugu kamili lenye kujumuisha zaidi ya wanaume elfu moja.

Kundi hilo linalojulikana kama Mkutano wa Msafara wa Wanaume linaundwa na takriban wanaume wengi na baadhi ya wanawake likigharimiwa na serikali ya Norway na Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa.

Hapo mwaka 2003 kundi hilo liliadhimisha siku 16 za kila mwaka za Harakati Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia ambayo ni kampeni ya kimataifa yenye kutaka kukomeshwa kwa ukatili dhidi ya wanawake na watoto na ambayo hufanyika kuanzia tarehe 25 mwezi wa Novemba hadi tarehe 10 mwezi wa Desemba kwa njia ya aina yake.

Wanaume kutoka Kenya, Zambia na Ethiopia walikutana katika mji mkuu wa Malawi Lilongwe baada ya kusafiri kwa basi.Wakiwa njiani wanaume hao husimama katika kila kijijiji na kuwacha ujumbe kwamba ukatili dhidi ya wanawake ni uharibifu na kwamba wanaume ndio wenye nguvu na wajibu wa kukomesha ukatili huo.

Wisdom Samu ni mmojawapo ya watu wanaosafiri na kundi hilo kila mwezi wa Desemba kuwaelimisha wanaume vijijini nchini Malawi. Hapo mwaka 2011 mke wake alifariki baada ya kujifunguwa mtoto wao wa saba.Kwa kupitia kundi hilo alikuja kutambuwa yeye ndie aliepaswa kulaumiwa kwani alikuwa hamruhusu mke wake huyo kutumia uzazi wa majira kwa sababu alitaka kuwa na watoto wengi.

Nalo taifa la Afrika magharibi la Mali hatua kwa hatua limekuwa likisonga mbele katika kuwahusisha wanaume zaidi katika masuala ya uzazi wa majira.

Repoti ya nchi hiyo ya Malengo ya Maendelo ya Milinia iliotolewa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa hapo mwaka 2010 imesema kwamba idadi ya vifo vya uzazi imeshuka kutoka 582 hadi kuwa 464 kwa kila uzazi wa watoto 100,000 wakiwa hai kati ya mwaka 2001 hadi mwaka 2008.

Hali hiyo imetokana na kampeni kubwa ya kuwahusisha wanaume katika uzazi wa majira.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Kuilinda na Kuindeleza Familia Mountaga Toure miaka kumi iliopita zahanti yake ilioko Bamako ilikuwa tu ikipokea wanawake lakini hivi sasa wanawake wamekuwa wakisindikizwa na waume zao jambo ambalo linaamanisha kwamba kile wanachokifanya kinafanikiwa.Wanaume hushajiishwa kuzungumzia mambo ambako daima yalihesabiwa kuwa ni mwiko.

Hayo ni mabadiliko makubwa katika nchi ya Kiislamu kama Mali iliojikita kwenye misingi ya dini hiyo.

Mwandishi: Mohamed Dahman/IPS
Mhariri: Iddi Ismail Ssessanga