Wanasiasa wa FARC wasitisha kampeni zao Colombia
10 Februari 2018Baada ya kusaini makubaliano ya amani ambayo yalimaliza vita vilivyodumu miaka 52, wafuasi wa lililokuwa kundi la waasi wa FARC waliunda chama kipya cha kisiasa mwaka wa 2017.
Waasi hao wa zamani waliamua kutumia herufi hizo za FARC kuwa jina la chama chao cha kisiasa, huku wakibadilisha tu maana ya Revolutionary Armed Forces of Colombia na kujiita Common Alternative Revolutionary Force. Wagombea wa FARC wamekuwa wakifanya kampeni za uchaguzi wa bunge utakaoandaliwa Machi na wa urais mwezi Juni.
Mgombea wa umakamu rais Imelda Daza amesema wamesitisha kampeni zao hadi serikali itakapowahakikishia usalama. Rais Juan Manuel Santos amelaani mashambulizi hayo akiwataka watu kufanya maandamano ya amani. Karibu asilimia 80 ya Wacolombia wanakipinga chama cha FARC.
Tangu walipoanzisha kampeni zao chini ya wiki mbili zilizopita, waasi hao wa zamani wamekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa makundi yenye hasira na maandamano, hali inayothihirisha changamoto za maridhiano ambazo bado ziko Colombia baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani mwaka wa 2016 kumaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu zaidi katika bara la Amerika Kusini.
Mgombea wa urais kwa tikiti ya chama cha FARC Rodrigo Londono alishambuliwa katika mojawapo ya mikutano yake ya kisiasa kwa kurushiwa mayai na mawe huku waandamanaji wakimuita "Muuaji!"
Waandamanaji nje ya mkutano wa kampeni wa mgombea wa seneti Luciano Marin kwa jina la utani Ivan Marquez, walichoma bendera nyeupe ya kundi hilo. Wagombea wengine wamefuatwa na kutishiwa.
Tangu kusainiwa kwa mkataba wa Amani, waasi hao wa zamani wamesalimisha silaha zao, na kuunda chama cha chao cha kisiasa na kuanza maisha mapya kama raia. Mgogoro huo wa miongo mitano kati ya waasi hao wa mrengo wa kushoto, makundi ya kijeshi na wanajeshi wa serikali, ulisababisha vifo vya karibu watu 250,000 na wengine 60, 000 kutoweka, huku milioni 7 wakipoteza makao.
Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa wengi nchini Colomboa wanaamini kuwa waasi wanapaswa kukiri uhalifu wao mbele ya tume maalum ya Amani kabla ya kuruhusiwa kugombea nyadhifa mbalimbali. Lakini mfumo wa mahakama haujaanza kusikiliza kesi na muafaka wa Amani unawapa waasi hao wa zamani viti 10 bungeni.
Waasi hao wa zamani wanapendekeza kuwa chama chao kinapaswa kuangazia masuala mengi ambayo ndiyo yaliyoanzisha mgogoro, kama vile ukosefu wa uswa na haki za mashamba.
Hadi sasa, ahadi za serikali za kupambana na mageuzi kama vile kuimarisha mazingira ya wakulima maskini zimecheleweshwa, na sehemu nyingine za muafaka huo zimebadilishwa na bunge.
Mwandishi: Bruce Amani/AP/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo